April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya NMB yachangia milioni 27/- kutatua changamoto Elimu na Afya Wilaya ya Ubungo

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Benki ya NMB imetoa vifaa mbalimbali vya afya na vya shule vyenye thamani ya Sh.milioni 27 kwa Hospitali ya Wilaya ya Ubungo, Shule ya Msingi Kwembe na Shule ya Sekondari Urafiki ikiwa ni muendelezo wa benki kuchangia katika maendeleo ya jamii zinazoizunguka.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo, Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard alisema wamekabidhi jumla ya vitanda 10 vya kulalia wagonjwa, vitanda vitano vya kujifungulia, mashine 15 za kupimia presha na mapazia 10 ya kutenganisha wodi. Kwa upande wa Shule ya Msingi Kwembe walipata viti na meza 35 za walimu huku Shule ya Urafiki wakipata meza na viti 110 kwaajili ya wanafunzi.

Meneja huyo aliongeza kuwa mbali na mengi yanayofanywa na serikali kwaajili ya wananchi, wao kama wadau wa maendeleo wanao wajibu wa kuendelea kuchangia katika jamii kwani jamii ndio chanzo cha mafanikio mengi ambayo benki hiyo imekuwa ikiyapata.

Akizungumza wakati wa kupokea vifaa hivyo, mgeni rasmi wa hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kheri James alisema kuwa Benki ya NMB inastahili pongezi kwani wamekuwa karibu sana sio tu kwa Wilaya ya Ubungo bali kwa wilaya mbalimbali nchini na wamekuwa wakisaidia sana hususani katika Sekta ya Elimu na Afya.

“Nitoe wito wangu kwa watumishi wa hospitali hii na walimu wa shule zinazopokea vifaa hivi, vifaa hivi vikawe chachu ya maendeleo ya sekta hizi. Tuvitumie vyema kwa maslahi mapana ya wananchi tunaowahudumia ili kila akifika kupata huduma akute vifaa hivi vikiwa katika hali nzuri na vitunufaishe,” aliongeza Mhe Kheri.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo,Jaffari Nyaigesha aliishukuru Benki ya NMB huku akiwaasa wananchi kuwa chachu ya kuhakikisha misaada hiyo inatumika vyema na inatunzwa katika hali nzuri ili iwanufaishe wengi zaidi.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Ubungo, Dk. Imani Mwanang’ombe alisema kuwa kwa misaada hiyo hospitali hiyo itakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa zaidi ya 250 kwa wiki hivyo kupelekea kuwa na uwezo wa kuhudumia wananchi zaidi ya 1,000 kwa mwezi huku idadi hiyo ikitazamiwa kuongezeka baada ya kukamilika majengo mengine ya hospitali hiyo Agosti mwaka huu.

Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard (wapili kushoto) akimkabidhi Mkuu wa wilaya ya Ubungo, Mhe. Kheri James (wapili kulia) moja ya viti 35 vya walimu kwa shule ya Msingi Kwembe na Shule ya sekondari Urafiki katika Hospitali ya wilaya ya Ubungo. Kushoto ni Meneja wa NMB tawi la Ubungo Plaza, Sylvester Ngowi na kulia ni Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispa ya Ubungo, Mhe. Jaffar Juma Nyaigesha.
Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard (wapili kushoto) akimkabidhi Mkuu wa wilaya ya Ubungo, Mhe. Kheri James (wapili kulia)moja ya mashine ya presha katika Hospitali ya wilaya ya Ubungo. Kushoto ni Meneja wa NMB tawi la Ubungo Plaza, Sylvester Ngowi na kulia ni Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispa ya Ubungo, Mhe. Jaffar Juma Nyaigesha.