May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya NBC yazindua Jamii Akaunti

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online,Dar

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua rasmi huduma mpya ya kibenki ijulikanayo kwa jina ‘NBC Jamii Akaunti’ ambayo ni mahususi kwa ajili ya taasisi zisizo za Kiserikali (NGOs), taasisi zinazotegemea misaada, taasisi zinazotoa misaada kwa jamii, taasisi za kidini na taasisi nyingine zenye agenda zinazofanana na hizo.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa huduma hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam hii jana, Meneja wa Huduma hiyo kutoka benki ya NBC, Mwinyiusi Hamza alisema huduma hiyo inalenga kuzaisaidia taasisi hizo ili ziweze kupata huduma za kibenki pasipokuwa na makato yoyote.

“Kupitia NBC Jamii Akaunti NGOs na taasisi zinazotegemea misaada kwa sasa zitaweza kupokea, kutunzaji fedha za miradi kutoka kwa wahisani bila makato ya mwezi huku wakiweza kufuatilia kila muamala unaofanyika,’” alisema na kuongeza;

“Pia kwa upande wa taasisi za kidini kwa maana ya makanisa na misikiti kupitia NBC Jamii Akaunti kutakuwa na urahisi zaidi wa upokeaji wa sadaka na zaka pamoja na michango mingine bila kusahau utunzaji wa fedha za miradi toka kwa wahisani na wadhamini wa taasisi hizi za kidini’’ alifafanua.

Maofisa waandamizi wa Benki ya NBC wakiongozwa na Mkuu wa Kitengo cha Wajasiliamali Bw Mussa Mwinyidaho (Katikati) wakizindua rasmi huduma mpya ya benki hiyo ijulikanayo kwa jina NBC Jamii Akaunti ambayo ni mahususi kwa ajili ya Taasisi zisizo za Kiserikali (NGOs) na taasisi za kidini wakati wa hafla fupi iliyofanyika jijini Dar es Salaam hii leo. Wengine ni Mkuu wa Kitengo cha Wateja wa Kati wa benki hiyo Bw Moses Minja (Kushoto) na Meneja wa Huduma hiyo Bw Mwinyiusi Hamza.

Alisema wadhamini, waumini na wahisani wanaweza kuweka fedha moja kwa moja kwenye Akaunti ya NBC Jamii ya taasisi husika kupitia njia mbalimbali na rahisi ikiwemo kutumia Huduma ya NBC Kiganjani kutoka kwenye Akaunti ya mtoaji kwenda moja kwa moja kwenye akauti ya taasisi husika ya NBC Jamii.

“Pia wanaweza kuweka fedha zao kupitia ATM za NBC zinazopokea fedha na kuweka fedha hizo moja kwa moja kwenye akauti ya taasisi husika ya NBC Jamii. Pia wanaweza kutumia mawakala wa NBC (NBC Wakala) na kuweka fedha hizo moja kwa moja kwenye akauti ya taasisi husika ya NBC Jamii. Njia nyingine ni pamoja na kutumia matawi yetu pamoja na simu za mikononi’’ alitaja.

Akizungumzia baadhi ya faida za akaunti hiyo kwa walengwa, Mkuu wa Kitengo cha Wajasiliamali, Mussa Mwinyidaho alisema pamoja na mambo mengine inawarahisishia wamiliki wa akaunti ufuatiliaji wa vitabu vya taasisi husika kupitia rekodi ya miamala isiyoingiliwa na makato.

Baadhi ya wageni waalikwa kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo taasisi zinazotegemea misaada, taasisi zinazotoa misaada kwa jamii, taasisi za kidini, mabalozi na wawakilishi wa mataifa wahisani wakifuatilia uzinduzi wa huduma hiyo.

“Zaidi kupitia akaunti hii wamiliki wataweza kufanya malipo kwa watu wengi kwa mara moja kupitia Huduma ya NBC Business Internet Banking. Pia wataweza kupokea taarifa za miamala ya fedha inayoingia na inayotoka sambamba na kupatiwa kitabu cha hundi bure.” Aliongezea.