May 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya KCB yavuka uzania wa trilioni moja

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

KUIMARIKA kwa uchumi na kuimarisha uendeshaji wa Benki ya KCB Tanzania hasa kwa kutumia teknolojia ya kidigitali kufikisha huduma kwa wateja, kumefanikisha benki hiyo kuweka rekodi kwa kufikia mali zenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni moja hadi kufikia kipindi cha robo tatu ya mwaka 2022.

Hayo ameyasema Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya KCB, Cosmas Kimario wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.

Amesema hatua hiyo inaipa uwezo benki kuongeza kasi ya utoaji huduma kwa wateja na kutekeleza mipango ya kukuza biashara.

“Benki hii imefikia kiwango cha uzani wa mali wa zaidi ya trilioni moja, hivyo beki hii inakuwa miongoni mwa mabenki makubwa zaidi nchini katika utoaji wa huduma kwa wateja wake na hii itatusaidia sisi kama benki kuendelea kuwahudumia vizuri wateja wetu na kwa kiwango cha juu zaidi,”amesema.

“Huduma kama Intanenti Benki, Mobile Banking, na njia za malipo (POS) zimeendelea kuongeza ufanisi wa huduma kwa wateja wetu, mapaka sasa asilimia kubwa ya miamala ya benki inafanyika nje ya matawi yetu, jambo ambalo limeongeza ufanisi,”amesema.

Kimario amesema mafanikio hayo pia yametokana na mikakati ya Benki kukuza huduma na kuimarika kwa mazingira ya biashara nchini.

Kimario amesema sekta ya benki imeanza kuimarika tena baada ya kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO-19 mwaka 2021.

“Biashara nyingi ziliweka mikakati ya kujipanua hasa baada ya athari za UVIKO-19 na matunda yake yameanza kuonekana, sisi pia imetusaidia kupata uzani imara na kuwahudumia wateja wetu kwa ukaribu zaidi”

Mbali na hayo, Kimario amesema uwekezaji katika rasilimali watu ni chachu nyingine iliyosababisha kuleta mafanikio hayo.

“Tumeendelea kuwekeza katika kuboresha na kukuza rasilimali watu ili kuongeza ufanisi, lakini zaidi tumefanikiwa kupunguza gharama za uendeshaji hadi asilimia 49 kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita ” alisema Kimario.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya KCB, John Ulanga amesema Benki imeendelea kukua tangu mwaka 1997 ilipoanzishwa.

“Benki ina mipango ya kujipanua zaidi ili kuweza kuwafikia Watanzania wengi zaidi ambapo tuna mkakati wa kuongeza matawi matano ndani ya miaka miwili ijayo kwenye mikoa mbalimbali ambayo bado hatujaifikia “

Amesema Tangu kuanzishwa kwa benki hiyo mipango yao mikuu ni kukua na mwaka huu wanafurahia ukuaji huo wa kufikia trilioni moja kwa sababu kwa mipango yao yote mwisho wa mwaka huu walitakiwa tufikie mali zenye thamani takribani bilioni 800, lakini wamefikia trilioni moja kabla ya miaka miwili mbele.

Naye Mkurugenzi wa fedha, Willis Mbatia amesema kwenye benki hiyo ya KCB utoaji wa mikopo umeongezeka kutoka sh.bilioni 330 mwaka 2017 hadi bilioni 623 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 88.

Pia Mbatia amesema benki inatarajia kupunguza mikopo chechefu hadi chini ya asilimia 3 kufikia mwisho wa mwaka huu.

Mbatia amesema mali zimekua kutoka sh. bilioni 508 mwaka 2017 hadi kufikia trilioni 1.04 Septemba 2022 sawa na ongezeko la asilimia 103.

“Uwiano wa mikopo chechefu umeshuka kutoka asilimia 17.51 mwaka 2017 hadi asilimia 3.16 mwaka huu”

Kuhusu amana za wateja, Mbatia amesema zimeongezeka kutoka sh. bilioni 318 mwaka 2017 hadi bilioni 646 mwaka huu sawa na ongezeko la asilimia 103.

Mbatia ameongeza kwamba, Faida kabla ya kodi kufikia Septemba 2022 ilikuwa bilioni 22.4 na kua ni ongezeko la asilimia 39 ukilinganisha na kipindi kama hicho cha mwaka 2021. Faida hii kwa kila robo mwaka imekuwa bilioni 6.9, bilioni 7.7 na bilioni 7.8 kwa robo ya kwanza, ya pili na ya tatu mtawalia.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya KCB Tanzania, Cosmas Kimario akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kutangaza mafanikio ya benki kufikia uzania wa mali wa trilioni moja.Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya KCB, John Ulanga na Willis Mbatia, Mkuu wa Fedha wa KCB (mwisho Kulia), Kaimu Mkuu wa Masoko, Uhusiano na Mawasiliano wa KCB, Shose Kombe (mwisho kushoto). Mafanikio hayo yanaipa benki hiyo nafasi ya kutanua wigo wa huduma hapa nchini.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya KCB, John Ulanga akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kutangaza mafanikio ya benki
kufikia uzania wa mali wa trilioni moja.Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa KCB, Cosmas Kimario na Mkuu wa Fedha, Willis Mbatia. Kaimu Mkuu wa Masoko, Uhusiano na Mawasiliano wa KCB, Shose Kombe (mwisho kushoto). Mafanikio hayo yanaipa benki hiyo nafasi ya kutanua wigo wa huduma hapa nchini.