May 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya Azania yatoa mikopo ya trekta kwa wakulima

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

KATIKA kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita za kuboresha shughuli za wakulima nchini, benki ya Azania imeanza kutoa mikopo ya zana bora za kilimo kwa wakulima wa tumbaku Mkoani hapa ili kuwainua kiuchumi.

Akikabidhi mkopo wa trekta kwa mmoja wa wakulima wa Mkoa huo Masudi Yasin, mkazi wa Kata ya Igigwa, wilayani Sikonge, kwenye maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD), Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amepongeza benki hiyo kwa kuunga mkono juhudi za serikali kwa vitendo.

Alibainisha kuwa taasisi za fedha zina mchango mkubwa sana katika kuboresha shughuli za wakulima na kuinua maisha yao, hivyo akawahakikishia kuwa serikali itaendelea kuwapa ushirikiano ili kufanisha utekelezaji majukumu yao.

‘Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ina nia ya dhati ya kuinua wakulima nchini, ndiyo maana imetenga bajeti ya kutosha mwaka huu ili kuboresha sekta hii’, alisema.

Meneja wa Benki hiyo anayeshughulikia Kilimo Agustin Matutu alisema wamejipanga vizuri kuhudumia wakulima wote kwa kuwapatia mikopo ya trekta na zana nyingine za kilimo kwa riba nafuu.

Aliongeza kuwa kwa kutambua umuhimu wa sekta ya kilimo nchini wataendelea kushirikiana na serikali ili kuhakikisha malengo yake ya kuinua sekta hiyo yanatimia kwa manufaa ya wananchi.

Naye Afisa Mahusiano wa Benki hiyo Denis Sebastian alibainisha kuwa taasisi hiyo ni mdau mkubwa wa wakulima na wafugaji nchini hivyo wanatoa mikopo hiyo ili kuwasaidia kutimiza malengo yao.

Alisema mikopo hiyo inatolewa ndani ya wiki mbili tu na masharti yamerahishwa sana ili kuwezesha wote wanaoomba zana hizo kuzipata ndani ya muda mfupi ili kuendelea na shughuli zao.

Aliongeza kuwa hadi sasa wamepokea zaidi ya maombi 15 ya mikopo ya zana hizo na kuwahakikishia kuwa wote watapatiwa huku akitoa wito kwa wakulima wote wanaohitaji kuwezeshwa mikopo hiyo kupeleka maombi yao.

Akitoa neno la shukrani baada ya kukabidhiwa ufunguo na namba ya usajili ya trekta hilo, mkulima Masudi Yasin alipongeza benki hiyo kwa kumwezesha chombo hicho chenye thamani ya sh mil 111.7 na kubainisha kuwa alikuwa anakihitaji kwa muda mrefu sana.

Alifafanua kuwa awali alikuwa anashindwa kupata mavuno mengi kutokana na zana duni alizokuwa akitumia lakini sasa ana uhakika wa kulima ekari zaidi ya 94 na kuvuna zaidi ya kilo 53,000 za mazao ya alizeti, tumbaku na mahindi.

Masudi Yasin Kilyamanda (aliyevaa kofia) mkulima wa tumbaku katika kijiji cha Lufwisi, kata ya Igigwa Wilayani Sikonge Mkoani Tabora akiwa na Viongozi wa Benki ya Azania baada ya kukabidhiwa ufunguo na namba ya usajili ya trekta lenye thamani ya sh mil 111.7, alilokopeshwa na benki hiyo kwa ajili ya kufanikisha shughuli zake za kilimo cha tumbaku, alizeti na mahindi. Picha na Allan Vicent.