Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online DSM
Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imeendelea kuimarisha juhudi zake za kutoa elimu kwa wanafunzi mbalimbali wa Sekondari na Elimu ya Juu nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukuza Taaluma ya Uhasibu na kuongeza uelewa kuhusu majukumu ya Bodi hiyo.
Katika mwendelezo wa juhudi hizo, wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Baobab wametembelea NBAA na kupatiwa mafunzo maalum yaliyolenga kuwajengea uelewa mpana kuhusu shughuli za Bodi pamoja na fursa zilizopo katika Taaluma ya Uhasibu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Prof. Siasa I. Mzenzi , ameipongeza shule hiyo kwa jitihada za kuwawezesha wanafunzi wake kupata elimu ya vitendo nje ya darasa, hususan wale wanaosoma masomo ya biashara na Uhasibu.

Aidha, ameeleza kuwa NBAA iko wazi kwa wanafunzi wanaosomea masomo ya uhasibu, na aliwasisitiza wasibadilishe taaluma kwa kuwa tayari wana msingi mzuri wa uhasibu. Pia alielezea kuwa hata wanafunzi wa michepuo wa masomo mengine ambao hawajasomea Uhasibu wanaweza kujiunga na mitihani ya Bodi hiyo kuanzia ngazi ya awali na hatimaye kufikia sifa za kuwa wahasibu kitaaluma.
CPA Prof. Siasa Mzenzi amewasisitiza wanafunzi hao kufanya vizuri katika masomo yao ili kufikia malengo waliyojiwekea, alieleza kwamba Taaluma ya Uhasibu ina nafasi kubwa katika Taasisi mbalimbali kutokana na uhaba wa Wahasibu nchini.

Pia ameongeza kwa kuanzia ngazi za awali za masomo kunawasaidia wanafunzi kujengwa kitaaluma na kuwa wahasibu bora wa baadaye, huku akisisitiza umuhimu wa uadilifu, uaminifu na kufanya kazi kwa bidii bila kusimamiwa ili kuendeleza na kulinda hadhi ya Taaluma hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa NBAA, Magreth Kageya, amesema ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwa wanafunzi hao, kwani imewapa fursa ya kupata taarifa sahihi na muhimu kuhusu majukumu ya Bodi pamoja na mwelekeo wa Taaluma ya Uhasibu.

Naye mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Baobab, Stephen Mahundi, ameishukuru NBAA kwa kuwapatia wanafunzi elimu ya Uhasibu, akisema itawasaidia katika masomo yao ya sasa na kuwaandaa kufikia malengo yao.
Ziara hiyo ni miongoni mwa juhudi za NBAA za kuendelea kujenga kizazi cha wataalamu wa Uhasibu wenye uelewa mpana na uwezo wa kukidhi mahitaji ya soko la ajira la ndani na kimataifa na kukuza uchumi wa nchi.

More Stories
Mchengerwa akabidhi boti za kuimarisha huduma za chanjo
NMB yatwaa tuzo tano za Kitaifa za AOSH kwa mwaka wa Pili mfululizo
Waziri Ndejembi,Dkt.Ramokgopa wakubaliana kuimarisha Ushirikiano wa Nishati