May 27, 2022

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

AZAKI zatakiwa kutafuta fedha kwa maendeleo

Na Joyce Kasiki,Dodoma

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai amezitaka Asasi za Kiraia Nchini kuhakikisha zinatafuta fedha ndani na nje ya nchi ili ziweze kuleta maendeleo katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo kwa kuzingatia vipaumbele vya Taifa.

Spika Ndugai amesema hayo wakati akifungua maonyesho ya  Wiki Ya Azaki kwa mwaka 2021 yanayoendelea katika ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Maonyesho ya Wiki Ya Azaki kwa mwaka 2021 yameanza Oktoba 23 mwaka huu huku yakitarajiwa kuhitimishwa Oktoba 29 mwaka huu,maonyesho hayo yanaongozwa na kauli mbiu isemayo ‘Azaki na Maendeleo.’

Amesema,Asasi za Kiraia zinapaswa kushirikiana na Serikali katika kuleta maendeleo ya nchi kwa kuzingatia vipaumbele vya Taifa huku akisema ni lazima zifanye kila jitihada za kutafuta fedha ili ziweze kufikia malengo hayo.

Vile vile ameziasa  Asasi hizo  kutumia tafiti  na takwimu zitazosaidia kutoa majawabu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili watanzania .

Ndugai ameongeza kuwa Asasi zinatakiwa kuwa na mwenendo wa kukosoa viongozi wa Serikali pamoja na kuwapongeza wanapofanya vizuri utekelezaji wa majukumu yao kwa ajili ya maslahi ya watanzania wote.

Katika hatua nyingine Ndugai amezitaka Asasi za Kiraia kufanya kazi kwa  weledi, uadilifu na kwa kufuata miongozo na taratibu zilizowekwa katika uendeshaji wa Asasi hizo.

Kwa upande wake Rais wa FCS Dkt Stigmata Tenga amesema Bunge lina wajibu wa kuleta Mabadiliko Chanya na  kupitia upya Sheria ,taratibu na miongozo ambayo inaziongoza Asasi hizo  ili ziweze kushiriki vyema katika maendeleo ya Taifa.

Naye  Mkurugenzi  Mtendaji wa Wajibu Ludovick Utoh  amesema AZAKI ni zaidi ya mashirika kwani zinafanya kazi kubwa ya kuhakikisha nchi inasonga mbele kimaendeleo.