May 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (mwenye kofia nyeusi) akipata maelezo ya hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa mradi wa Chabula-Bugando kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele.

Aweso awaagiza wataalam mradi wa Chabula-Bugando

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

NAIBU Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amewaagiza wataalam wanaotekeleza mradi wa Chabula-Bugando utakaotumia chanzo cha maji ya Ziwa Victoria kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa hasa ikizingatiwa kwamba fedha ya utekelezaji wake inatoka kwa wakati.

Waziri Aweso ametoa agizo hilo alipokuwa katika ziara yake ya kukagua hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa mradi huo utakaonufaisha wakazi 16,000 kutoka Kata ya Chabula Wilayani Magu Mkoani Mwanza yenye vijiji vya Bugando, Chabula, Nyashigwe na Kongolo pamoja na kuzungumza na wataalam wanaoutekeleza mradi huo.

Aweso amesema, lengo la Serikali ya awamu ya Tano kupitia Wizara ya Maji ni kuwasogezea huduma ya maji safi na salama wananchi wake ili kuwaepusha na usumbufu wa kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo muhimu kwa maisha ya binadamu na viumbe hai.

Amesema kuwa, adhima ya Rais John Magufuli ni kumtua mama ndoo kichwani kwa kumsogezea huduma ya maji karibu ili kumuondolea kero iliyomsumbua kwa kipindi kirefu kwa kutembea masafa marefu kutafuta maji.

Amesema, hadi sasa Dkt. Magufuli ametoa zaidi ya shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuhakikisha mradi wa Chabula-Bugando unakamilika haraka ili wananchi wapate maji, hivyo Wizara hiyo itahakikisha mradi unakamilika kwa wakati.

“Tumesema sasa imetosha wananchi kuhangaika, hatuwezi tukawa na ziwa karibu hapa halafu wananchi walalamike hawana huduma ya maji safi, tunawahakikishia wananchi wote wa vijiji vya Bugando, Chabula, Nyashigwe na Kongolo kwamba mtapata maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria, huu ni mradi mkubwa na unatosheleza,” amesema Aweso.

Pia alielekeza ajira zitokanazo na ujenzi wa mradi huo kipaumbele cha kwanza kiwe kwa wananchi wa eneo la mradi ili waanze kupata manufaa hata kabla ya mradi kukamilika kwa kujiongezea kipato hivyo wananchi wa maeneo yote ya mradi kuhakikisha wanautunza na kuulinda ili waendelee kunufaika kwa miaka mingi ijayo kama ulivyosanifiwa na hasa ikizingatiwa kwamba Serikali inatumia fedha nyingi kwenye ujenzi wake.

“Wananchi shirikianeni kuulinda na kuutunza huu mradi sanjari na kuhakikisha mnatunza chanzo cha maji ili uwe endelevu na muweze kunufaika nyinyi na vizazi vyenu,” amesema Aweso.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli amemshukuru Rais Magufuli kwa kuwapatia mradi huo wa maji na alipongeza jitihada za Wizara ya Maji katika kuhakikisha miradi inajengwa kwa viwango na inakamilika kwa wakati.

Akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa mradi, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele amesema, mradi unatekelezwa kwa ushirikiano wa wataalam wa ndani kutoka Wakala ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na MWAUWASA.

Mhandisi Msenyele amesema kuwa, mradi unajengwa kwa miezi tisa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.69 bila VAT ambazo zinahusisha ujenzi wa chanzo chenye uwezo wa kuzalisha lita za ujazo 75,000 kwa saa, ulazaji wa bomba kutoka ziwani, ujenzi wa tenki la lita 250,000 na ulazaji wa bomba za usambazaji.

Amebainisha kwamba, tayari wamepokea kiasi cha shilingi milioni 550 kutoka Wizara ya Maji kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo ambao alisema ulianza kutekelezwa Aprili, 2020 na utakamilika Desemba mwaka huu.