June 21, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Asakwa kwa tuhuma za kumuua pacha mwenzie

Na Mwandishi Wetu,Mwanza

Kulwa Medard(14),mkazi wa Kijiji cha Bugatu,Wilaya ya Magu mkoani Mwanza anasakwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za mauaji ya pacha wake Dotto
Medard(14)mkazi wa kijiji hicho.

Akizungumza Juni 19,2026 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,DCP.Wilbord Mutafungwa, amesema tukio hilo lilitokea Juni 14,2026 majira ya saa 11.00 jioni katika Kitongoji cha Nyandanda, Kijiji cha Bugatu, Kata ya Ng’haya, Tarafa ya
Ndagalu, wilayani Magu.

Ambapo inadaiwa pacha hao wawili, wakitokea machungoni,walianza mchezo ambao baadaye uligeuka kuwa ugomvi na kuanza kupigana kwa kutumia fimbo kitendo kilichosababishia Dotto kujeruhiwa kichwani upande wa kushoto juu ya jicho na hatimaye kusababisha kifo chake.

DCP.Mutafungwa ametoa wito kwa yeyote mwenye taarifa za mahali alipo
mtuhumiwa kuzifikisha haraka katika kituo chochote cha polisi au kutoa taarifa kwa mamlaka nyingine za serikali ili akamatwe na kuchukuliwa hatua stahiki za sheria.

Hata hivyo ametoa rai kwa wazazi,walezi na jamii kwa ujumla kuwa makini na kufuatilia kwa karibu michezo ya watoto wao ambayo ni hatarishi kwa usalama wao na wengine.

“Michezo inayohusisha silaha za jadi au vitu hatarishi kama fimbo na mawe inapaswa kupigwa marufuku mara moja ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza,”amesema DCP.Mutafungwa.