May 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Apple, Google kuja na programu ya kuwatambua wenye Corona

Na Mwandishi Wetu,

WASHINGTON, Kampuni ya Apple Inc na Google zinatarajia kuja na mpango kabambe unaolenga kuongeza teknolojia katika majukwaa ya simu janja zao ambayo itawapa tahadhari watumiaji wa simu hizo ikiwa wamegusana na mtu mwenye virusi vya corona (COVID-19).

Kwa mujibu wa tovuti ya Bloomberg, programu hiyo itakuwa inataka watu waingie kwenye mfumo maalum, lakini pia ina uwezo wa kufuatilia karibu theluthi ya idadi ya watu duniani.

Teknolojia hiyo, inayojulikana kama ufuatiliaji wa mawasiliano imeundwa kupunguza kuenea kwa ugonjwa huo, kwa kuwaambia watumiaji wanapaswa kujitenga au kuchukua hatua mapema baada ya kugusana na mtu aliyeambukizwa.

Washirika katika ufanikishaji wa teknolojia hiyo, Kampuni ya Silicon Valley ilieleza jana kuwa, wanaunda mfumo wa teknolojia kupitia mifumo ya iOS na Android kwa hatua mbili.

Mosi ni ifikapo katikati ya mwezi Mei, mwaka huu kampuni hiyo itaongeza uwezo kwa simu janja za iPhones na Android kwa kuongeza mfumo wa viwasilisha taarifa kupitia programu tumishi za mamlaka za umma katika sekta ya afya.

Pia kampuni itakuja na mpango kazi wa kuwezesha sekta za afya kuwa na uwezo wa kusimamia programu tumishi hiyo kupitia uwasilishwaji wa taarifa.

Kwa mujibu wa Bloomberg, hii inamaanisha kuwa, kama mtumiaji atapimwa na kukutwa yupo ‘positive’ dhidi ya Covid-19 na kuongeza taarifa katika programu tumishi ya afya, mtu ambaye atakutana naye baadae atajulishwa juu ya hali yake kupitia progaramu hiyo. Kipindi hicho kitadumu kwa siku 14, lakini kwa mujibu wa taarifa mawakala wa sekta ya afya wanaweza kuweka muda wao wa kupata taarifa kadri wanavyoona.

Hatua ya pili itachukua muda mrefu. Katika miezi ijayo, kampuni zote mbili zitaongeza teknolojia moja kwa moja kwenye mifumo yao ya kufanya kazi. Programu hii ya kutafuta mawasiliano inafanya kazi bila kupakua programu.

Watumiaji lazima waingie, lakini njia hii inamaanisha watu wengi zaidi wanaweza kujumuishwa.

Apple’s iOS na Google’s Android ina watumiaji karibu bilioni 3 kati yao, hii ikiwa ni zaidi ya theluthi ya idadi ya watu duniani.

Zaidi jipatie nakala ya gazeti la Majira…