May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Airpay kuchochoea kasi ya ukuaji uchumi zanzibar

Na Penina Malundo

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na mipango Zanzibar Dk. Saada Mkuya Salum, amesema kuwa uamuzi wa kampuni ya Airpay kuanzisha kituo cha teknolojia nchini utachochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Pia alitoa rai kwa taasisi mbalimbali za serikali kutumia mifumo ya wakala wa serikali mtandao na kuitaka taasisi hiyo kuhakikisha usalama wa mifumo inayoanzishwa ili kupunguza changamoto za kifedha.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Kampuni hiyo ya AirPay Tanzania ulioenda sambamba na uzinduzi wa Mtandao wa Idara ya Mashirikiano baina ya serikali na sekta binafsi(PPP), amesema mfumo huo utakuza uchumi wa nchi hasa ikizingatiwa kuwa serikali ya Zanzibar inatekeleza sera za uchumi wa bluu.

Amesema Airpay itaweza kusaidia kupunguza matumizi ya cash sokoni na badala yake kutumia mtandao ambapo utasaidia kuiwezesha fedha kutokuchakaa na kuingiza serikali hasara ya kuzalisha fedha mpya kila mara.

Dkt. Saada amesema mfumo huo utawasaidia wajasiriamali wadogo wadogo kutumia mfumo wa kidigital wa kufanya malipo pamoja na kuongeza usalama wa fedha.

“Pongezi na shukrani kwa serikali ya India kwa kuendelea kuisaidia Zanzibar na Tanzania jambo linalokwenda kuimarisha zaidi uhusiano mzuri”amesema.

Amesema kipindi kirefu serikali ya Zanzibar ikijaribu kutafuta suluhisho kutoka katika matumizi ya fedha taslim na kwenda kulipia kimtandao ambao hakuna sababu ya kubeba fedha kwa ajili ya kununua bidhaa au kufanya malipo mbalimbali.

Kwa Upande wake Waziri wa nchi, ofisi ya rais, kazi, uchumi na uwekezaji Mudrik Ramadhan Soraga amesema kuwa mfumo wa malipo uliozinduliwa utachangia ukuaji wa uchumi na kurahisisha ukusanyaji wa mapato ya serikali.

Amesema kuwa mfumo huo unajumuisha makundi yote yanayohusika na biashara, ujasiriamali na uhaulishaji wa fedha na mfumo huo sio mgeni na nchi mbalimbali unatumia na lengo mahsusi serikali kuwa na takwimu halisi ya mwenendo wa uchumi.

“Katika mazingira yetu ya Zanzibar zaidi ya asilimia 70 ya wafanyabiashara bado hawajarasimishwa hivyo hakuna takwimu halisi za uchagiaji wa kodi kwa wafanyabiashara hao wakiwemo wakubwa, wakati na wadogo”amesema Soraga.

Naye Waziri wa biashara na viwanda Omar Said Shabani, amesema mfumo huo wa air pay utawezesha mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara katika kufanya malipo lakini si kwa wafanyabiashara pekee hata watoa huduma.

Amesema mfumo huo utaleta mapinduzi makubwa katika mazingira mazuri ya biashara, ufanyaji wa malipo na mambo mingine na wizara yake inatarajia kufanya maonesho ya kibiashara hivyo mfumo huo utumike katika ulipaji ambapo huduma hiyo ni salama.

Naye Mwazilishi mweza wa Airpay Tanzania Yasmin Chali, amesema wameamua kuwekeza Zanzibar kutokana na umahiri wake kwenye biashara na uvumbuzi wa masuala mbali mbali hivyo watajitahidi kuhakikisha uwekezaji wao unawanufaisha watu wote.

Amesema kuwa katika kufuikia lengo hilo watahakikisha wanatoa elimu ya matumizi jumuishi ya fedha ili kuwafanya wajasiriamali na watumiaji wengine wa huduma za kifedha kukua kibiashara lakini pia kupata suluhu juu ya masuala ya fedha.

Kwa upande wake Mwanzilishi wa Kampuni ya Airpay, Kunal Jhunjhunwala amesema lengo lao ni kutaka kumfikia mtu wa kawaida na kwa jinsi Zanzibar inavyoendelea wameona ni mahali sahihi kuwekeza, kwani huduma hii bora itatolewa katika nchi zaidi ya 12,” amesema.