Na Martha Fatael,TimesMajiraOnline
MILIMA imeendelea kuwa nguzo muhimu ya maisha duniani kwa kutoa maji, kuhifadhi bioanuwai, na kubeba urithi wa kitamaduni. Hata hivyo, kwa miaka mingi masuala kuhusu milima hayajapata kipaumbele cha kutosha katika mazungumzo ya kimataifa ya tabianchi.
Katika mkutano wa 30 wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP30), unaofanyika Belém, Brazil, suala hili hatimaye limepata uzito wa kipekee, huku nchi kama Kyrgyzstan zikipigania kutambuliwa rasmi kwa milima kama maeneo nyeti yanayohitaji ufadhili wa haraka.
Baku–Belém roadmap yaweka milima katika kipaumbele
Kwa mujibu wa nchi ya Kyrgyzstan, milima imepewa umuhimu katika ramani ya mwongozo ya Baku–Belém (ni njia ya kimaelezo ya miongozo na maazimio yanayounganisha matokeo ya Mikutano ya COP29 (Baku, Azerbaijan) na COP30 (Belém, Brazil) inayounganisha matokeo ya COP29 na COP30. Ndani ya hati hiyo, milima inatajwa kuwa chanzo kikuu cha maji duniani, hifadhi ya bioanuwai, na maeneo ya urithi wa kitamaduni yanayohitaji kulindwa.
Naibu Mwenyekiti wa Serikali, nchi ya Kyrgyzstan Edil Baisalov, amesema katika kikao cha hoja za urekebishaji wa tabianchi, amesisitiza umuhimu wa milima katika ulinzi wa mazingira na changamoto zinazotokana na kupuuzwa kwa milima katika upangaji wa ufadhili wa tabianchi. Alionyesha kuwa milima ni rasilimali muhimu inayohusiana na maji, bioanuwai, na urithi wa kitamaduni wa mamilioni ya watu duniani.

“Milima ni uti wa mgongo wa mazingira yetu. Inatoa maji, inalinda bioanuwai na inadumisha utamaduni wa mamilioni ya watu. Hata hivyo, imepuuzwa kwa muda mrefu katika upangaji wa ufadhili wa tabianchi.” Amesema Baisalov
AHADI ZA COP29 KUHUSU MILIMA NA KILE KILICHOKWAMA KUTEKELEZWA
Katika Mkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP29) uliofanyika Baku, Azerbaijan, nchi wanachama zilitoa ahadi kadhaa za kuimarisha ulinzi wa milima. Ahadi hizo ziliweka msukumo mpya kwa nafasi ya milima katika jitihada za kimataifa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, zikiwemo kuanzishwa kwa Mfumo wa Kimataifa wa Ufuatiliaji wa Ikolojia za Milima, kuunda dirisha maalum la ufadhili ndani ya Mfuko wa Tabianchi wa Umoja wa Mataifa (Green Climate Fund – GCF), na kuandaa ripoti ya pamoja ya kimataifa kuhusu kuyeyuka kwa barafu, mmomonyoko wa udongo na upotevu wa maji katika maeneo ya milimani.
Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti mwaka mmoja baadaye. Kufika COP30, ahadi nyingi zilikuwa hazijatekelezwa. Hakukuwa na dirisha maalum la ufadhili lililoanzishwa rasmi ndani ya GCF, huku mfumo wa ufuatiliaji wa ikolojia za milima ukikwama kutokana na kutokuwepo kwa makubaliano ya kifedha kati ya nchi zinazochangia na zile zinazoathirika. Vilevile, ripoti ya utafiti wa pamoja haikuandaliwa wala kuwasilishwa, licha ya muda wa kutosha kutolewa katika makubaliano ya COP29.
Mratibu wa Masuala ya Tabianchi kutoka nchi ya Kyrgyzstan, Aizada Abakirova, ameeleza kwenye kikao cha wadau wa milima COP30 ameeleza hali iliyopo kufuatia makubaliano ya COP29 Baku, akisisitiza changamoto za utekelezaji wa ahadi zilizotolewa. Alionyesha kuwa bila hatua thabiti na ufadhili ulioahidiwa, nchi zinazotegemea milima zinakabiliwa na hatari kubwa ya kupoteza vyanzo vya maji na bioanuwai.
“Tulitegemea kuona hatua thabiti kufuatia makubaliano ya Baku, lakini hakuna mifumo mipya iliyoanzishwa. Bila ufadhili ulioahidiwa, nchi za milima zinabaki kwenye hatari kubwa ya kupoteza vyanzo vyao vya maji na bioanuwai.” Amesema Abakirova
Mwakilishi wa Tanzania, Afisa wa Mazingira na Kilimo kutoka Wizara ya Kilimo, Juma Mndeme, alihudhuria kikao hicho cha pembeni (side event) ya milima kwenye COP30, akisisitiza changamoto zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa na athari zake kwa kilimo cha kahawa katika mikoa ya milimani. Alionyesha kuwa miradi ya adaptation ni muhimu ili kulinda kilimo na bioanuwai inayotegemea milima.
“Kahawa inategemea mvua za uhakika. Tunaona mabadiliko makubwa sana. COP29 ilituahidi utafiti na msaada, lakini hadi leo hatujaona chochote kinachotekelezwa kwenye mashamba yetu.”amesema Mndeme.
Aliongeza kuwa Tanzania inahitaji ushirikiano wa kimataifa na ufadhili thabiti ili miradi ya kulinda vyanzo vya maji na milima iweze kufanikishwa kwa manufaa ya wakulima na jamii zinazotegemea milima.
Mwenyekiti, Mtandao wa Wataalamu wa Tabianchi Afrika Mashariki (EACC) Prof. John Mugisha, ameonyesha hofu kuhusu athari zinazoongezeka kwa barafu za Kilimanjaro, Rwenzori na Mount Kenya, na umuhimu wa data sahihi za ufuatiliaji.
“Barafu za Afrika kama Kilimanjaro, Rwenzori na Mount Kenya zinayeyuka kwa kasi isiyo ya kawaida. Ucheleweshaji baada ya COP29 unatupunguzia uwezo wa kulinda jamii zetu.” Amesema Prof. Mugisha
Kwa kifupi, COP29 iliibua matumaini makubwa lakini utekelezaji ulibaki kuwa mdogo, na hivyo kusababisha nchi zinazotegemea milima kuingia COP30 zikiwa na matarajio mapya na shinikizo kubwa la kuhitaji hatua za haraka.
Hata hivyo, hadi kufika COP30, hakuna dirisha maalum la ufadhili lililoanzishwa rasmi ndani ya GCF, mfumo wa ufuatiliaji haukuanzishwa kutokana na kukwama kwa makubaliano ya kifedha na ripoti ya utafiti ilishindikana kuwasilishwa licha ya muda wa mwaka mmoja kupita
Kwa kifupi, COP29 iliibua matumainilakini utekelezaji ulibaki kuwa mdogo sana.
KAULI ZA WASEMAJI WA KIMATAIFA COP30
Athari za milima katika usalama wa maji na bioanuai
Katika kikao cha upande kilichoandaliwa na Mradi wa Urekebishaji wa Milimani (Adaptation at Altitude), wataalamu walionyesha wazi uhusiano wa karibu kati ya milima, maji na bioanuwai. Milima inatambulika kuwa vyanzo muhimu vya maji safi, ikolojia ya kipekee, na urithi wa kitamaduni. Kulinda milima ni hatua ya lazima katika mkakati wa kimataifa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mkurugenzi wa Ikolojia ya Dunia, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) Dkt. Maria Estevez, amesisitiza umuhimu wa milima katika usalama wa maji duniani na kuanzishwa kwa mifumo thabiti ya ufuatiliaji wa milima.
“Hakuna mafanikio ya kimataifa ya tabianchi bila kulinda milima. Nusu ya watu duniani wanategemea maji yanayotoka milimani. Ikiwa milima haitalindwa, usalama wa maji utadidimia.”amesema Dkt. Estevez
Mwakilishi, Andes Mountains Coalition, Cecilia Ramírez, Andes, Amerika Kusini
Ramírez alisisitiza madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwenye kilimo na mito, na umuhimu wa ushirikishwaji wa moja kwa moja wa jamii za milimani.
“Tunapoteza udongo, misimu ya kilimo imevurugika, na mito inapungua. Tunahitaji hatua, sio ahadi zinazojirudia.” amesema Ramírez
Mdau wa Mazingira, mkazi wa Moshi Amina Mwandazi, ameelezea changamoto za maji vijijini na umuhimu wa miradi ya ulinzi wa vyanzo vya maji inayoungwa mkono na fedha za kimataifa.
“Kuyeyuka kwa theluji kunachangia kupungua kwa maji kwenye vijito. Tunataka kuona fedha za kimataifa zikisaidia miradi ya kulinda vyanzo vya maji.” Amesema Mwandazi
Mkulima wa Kahawa Mwidini Juma, Moshi Vijijini, amebainisha athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwenye kilimo cha kahawa na umuhimu wa mipango madhubuti ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
“Kahawa inategemea mvua za uhakika. Tunaona mabadiliko makubwa sana. COP29 ilituahidi utafiti na msaada, lakini hadi leo hatujaona chochote kwa mashamba yetu.” Amesema Juma.
Mfanyabiashara mkazi wa Moshi mjini, Hawa Mrema, amesisitiza uhusiano wa mlima na utalii, na umuhimu wa kulinda Kilimanjaro kwa maslahi ya kiuchumi na jamii.
“Utalii wa Kilimanjaro unategemea afya ya mlima. Serikali inapaswa kusukuma ajenda hii kwa nguvu zaidri kimataifa.” Amesema Mrema.
Hitimisho
Ingawa COP30 imeipa milima nafasi ya kipekee, changamoto kubwa bado ni utekelezaji wa maazimio. Ahadi zilizotolewa Baku hazikutekelezwa kikamilifu, na sasa dunia inatazama kama Belém itakuwa mwanzo wa hatua za kweli.
Kwa jamii zinazotegemea milima kama Moshi, Himalaya, Andes na Rwenzori, kulinda milima si mjadala wa kisiasa tu, ni suala la maji, maisha na mustakabali wao.


More Stories
NMB ilivyosaidia Serikali kukusanya zaidi ya Sh trilioni 9.8
Serikali yaongeza nguvu kwa wachimbaji wadogo,yasisitiza usalama Migodini
REA imeleta mageuzi sekta ya nishati