May 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Afrika Kishirikiana kutatua changamoto ya usafirishaji bidhaa

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.) amesema Nchi za Afrika zimekubaliana kushirikiana katika kutatua changamoto mbalimbali za kibiashara ikiwemo usafirishaji wa bidhaa ndani ya Bara la Afrika ili kuiwezesha Sekta Binafsi ambayo ni injini ya ujenzi wa uchumi kufanya biashara kwa ufanisi.

Waziri Kijaji ameyasema hayo Septemba 06, 2023 wakati akishiriki Mkutano wa Watendaji Wakuu wanaohusika na Sekta ya Biashara na Uwekezaji wakati wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula (AGRF) kwa mwaka 2023 linalofanyika katika Kituo cha Mikitano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.

“ Kupitia AGRF, tumekubaliana kuanza kushughulikia changamoto kubwa zilizopo ikiwemo gharama kubwa za usafiri na usafirishaji bidhaa ndani ya bara letu na muda mrefu wa kusafiri kutoka nchi moja ya Afrika kwenda nchi nyingine”. Amesema Dkt. Kijaji.

Vilevile, amebainisha kuwa nchi hizo za Afrika zimekubaliana kila moja kuwekeza ndani ya nchi yake na kushirikiana ma nchi nyingine hususani katika usafiri wa ndege za mizigo ili ziweze kusafiri zaidi ndani ya Bara la Afrika nakufikia lengo la kufanya biashara kwa pamoja na kwa haraka.

Kwa upande wa Tanzania, Dkt. Kijaji amempongeza Rais wa Jamhuri ya Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ununuzi wa ndege ya mizigo ambayo itaanza kupunguza muda wa kusafirisha mizigo kutoka nchi moj ya Afrika kwenda nchi nyingine.

Dkt. Kijaji pia amesema katika kutatua changamoto hiyo Tanzania imeridhia Itifaki ya Biashara ya Huduma ya SADC ya 2012 yenye dhamira ya kuondoa changamoto wanazokumbana nazo wafanyabiashara nchini wanaposafirisha bidhaa kutoka nchi moja kwenda nchi zingine.

Vilevile alibainisha kuwa Tanzania imeanza utekelezaji wa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) ambapo imeanza kushirikiana na mataifa ya Afrika kuhakikisha miundombinu ya ufanyaji biashara inawekezwa nchini na bidhaa ya kwanza ya Kahawa iliuzwa kutoka Tanzania kwenda Senegal kupitia Mkataba huo.

Dkt. Kijaji pia amesema Tanzania ni moja ya mataifa ambayo yapo kwenye eneo linalohitaji kufanya biashara ya mizigo mingi ya kwenda nchi za Afrika hivyo inafanya jitihada mbalimbali ya kuboresha miundombinu ya usafiri kama reli ya kisasa ambayo itatoka Dar es Salaam hadi Kigoma, Burundi, DRC, na Dar es Salaam hadi Kigali Rwanda ili mizigo iweze kusafiri na kuwafikia wahitaji kwa muda muafaka.