May 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Afariki kwa kujifungia ndani na kujilipua na moto wa Petrol na familia yake

Na Esther Macha, timesmajira, Online,Mbeya

HAMIS Pius(41)mkazi wa mtaa wa Nyigamba Kata ya Itezi Jijini Mbeya amefariki dunia baada kujifungia ndani yeye na familia yake kisha kujilipua kwa moto wa petrol chanzo kikitajwa kuwa ni mgogoro wa ndoa baina yake na mkewe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Benjamin Kuzaga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa tukio hilo limetokea machi 8 mwaka huu majira saa 4.00 usiku katika maeneo ya Nyigamba , mtaa wa Itezi Jijini Mbeya .

Kamanda Kuzaga amesema kuwa mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Hamis
alifariki dunia baada ya kuungua moto baada ya kujifungia ndani ya chumba anacholala na mke wake aitwaye Rebelia Makoso (38) mkazi wa Nyigamba kisha kumwaga petrol na kuwasha moto.

Aidha Kuzaga amesema wakati wa tukio hilo, mke wa marehemu alipiga kelele kuomba msaada kwa mtoto wake aitwaye Mkeshilisi Hamis (21) ambaye alikuwa chumba kingine ambaye alikwenda kutoa msaada kwa kupiga teke mlango wa chumba na kisha kumuokoa mama yake lakini baba yake alikataa kutoka ndani na kupelekea kuungua hadi kupoteza maisha.

Hata hivyo uchunguzi wa awali wa tukio hilo umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi, majeruhi ambao ni mke na mtoto wa marehemu wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali Teule ya Ifisi iliyopo Mji Mdogo wa Mbalizi kutokana na majeraha ya moto waliyoyapata mwilini.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa jamii kuachana na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi.

Pia Kamanda Kuzaga ametoa wito kwa jamii kutatua migogoro yao ya kifamilia na ndoa kwa kukaa meza moja ya usuluhishi badala ya kuchukua maamuzi magumu kama hayo.