May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ADEM yafanya tafiti za tathimini matokeo ya mafunzo ya KKK kwa walimu ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji

Na Zena Mohamed,TimesMajiraOnline,Dodoma. 

WAKALA wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM)umesema kuwa Katika kipindi cha mwaka 2020/2021,umefanya tafiti mbalimbali zikiwemo za tathimini ya matokeo ya Mafunzo ya KKK kwa Walimu wa Darasa la III na IV yaliyofanyika Tanzania Bara, utekelezaji wa uthibiti ubora wa shule na utoaji wa mrejesho kwa walimu ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji katika shule za Msingi.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Novemba 15,2022 na Mtendaji Mkuu wa ADEM,Dkt. Siston Mgullah wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya wakala huo na vipaumbele vyake kwa mwaka wa fedha 2022/23

Dkt.Mgullah amesema kuwa tathmini hizo ni pamoja na Udhibiti wa majanga katika Shule za Sekondari Tanzania.

Ufuatiliaji wa utendaji kazi wa Wakuu wa Shule waliopata mafunzo ya Uongozi na Utawala katika Elimu, ufuatiliaji wa matokeo ya mafunzo ya Stashahada ya uongozi na usimamizi wa Elimu na tathmini ya athari za kozi ya Astashahda ya Uongozi, Usimamizi na Utawala wa elimu iliyofanyika katika mikoa minne.

Vilevile,Dkt.Mgullah amezungumzia Katika kipindi cha miaka mitano (2018- 2022),kuwa Wakala umetoa machapisho ya Moduli ya wajibu na majukumu ya Mjumbe wa Kamati na Bodi ya Shule,wajibu na majukumu ya Mjumbe wa Bodi ya Chuo cha Ualimu 2022.

“Moduli ya uthibiti ubora wa Shule wa ndani 2021 na uandaaji na usimamizi wa Utekelezaji wa Mpango wa Jumla wa Maendeleo ya Shule – 2018,”amesema.

Akizungumzia utekelezaji wa malengo ya ADEM kwa 2021/2022,amesema kuwa Wakala umedahili Walimu 1,839 katika mafunzo ya Stashahada ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu (DEMA) na Stashahada ya Uthibiti Ubora wa Shule (DSQA) ili kuwapa ujuzi na maarifa walimu katika usimamizi, ufuatiliaji na tathimini katika elimu.

“Wakala umetoa mafunzo ya muda mfupi kuhusu uthibiti ubora wa shule wa ndani, kwa Maafisa 3,860 (REOs, RAOs, DEOs, WEOs) ili kuwajengea uwezo wa kusimamia ufundishaji na ujifunzaji wenye kuleta tija katika elimu,

“Wakala umetoa mafunzo ya muda mfupi kuhusu uthibiti ubora wa shule wa ndani kwa walimu 7,612 ili kuwajengea uwezo wa kusimamia ufundishaji na ujifunzaji katika shule wanazosimamia,”amesema.

Pamoja na hayo Dkt.Mgullah pia  amezungumzia malengo ya wakala huo kwa mwaka 2022/2023 ambapo amesema kuwa wamedahili Walimu 2343 katika Kozi za CELMA, DEMA na DSQA, kuandaa Kiongozi cha Mwalimu Mkuu na kuandaa Mwongozo wa Utawala Bora kwa viongozi wa Serikali za Mitaa.

“ADEM imejipanga kutoa Mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Shule kwa Walimu Wakuu wapatao 17,000, kutoa mafunzo ya utawala Bora kwa wasimamizi wa elimu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa,”amesema.

Kwaupande wake Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amesema kuwa
Serikali inaweka fedha nyingi kwenye sekta ya elimu nchi nzima ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/23, sekta ya elimu pekee imetengewa Shilingi trilioni 5.8. Chuo hiki ni moja ya juhudi za Serikali za kusimamia ubora wa elimu.

“Fedha hizi ni nyingi ambazo zinahitaji usimamizi wa karibu, hivyo wale viongozi wa kwenye taasisi zinazosimamia elimu lazima wawe na ujuzi na mbinu nzuri za kusimamia maendeleo ya elimu ili tuweze kupata thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali,

“Viongozi wanaosimamia Taasisi za Elimu wanatakiwa wakasome katika chuo hiki ili wakapate ujuzi wakasimamie vizuri taasisi hizo. Natoa wito kwa waajiri kutosita kuwaruhusu viongozi wa taasisi za elimu kwenda kusoma ADEM,”amesema Msigwa.