May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TASAF yatatua changamoto sekondari ya Mang’oto

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online Makete

UJENZI wa bweni, nyumba nne za walimu na bwalo la chakula ambao umetekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Sekondari ya Mang’oto wilayani Makete umepunguza changamoto nyingi zilizokuwa zinakwamisha maendeleo ya elimu shuleni hapo.

Hayo yamesemwa na Mwalimu Mkuu wa Sekondari ya Mang’oto, Deonis Mgina, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na miradi hiyo iliyotekelezwa na TASAF ilivyochangia kuboresha kiwango cha elimuMgina amesema miradi ya TASAF imesaidia kutatua changamoto nyingi zilizokuwa zikikumba shule hiyo na kuzorotesha maendeleo ya elimu tangu ilipoanzishwa. Ametoa mfano akisema bweni hilo lina maji, vitanda, mazingira ambayo yanavutia wananfunzi kusomea katika shule hiyo.

Amesema kwa jinsi shule ilivyoanzishwa ilikuwa ya kutwa, lakini baada ya kuona wanafunzi wa kiume na kike wanaishi nyumba za kupanga mitaani, wazazi na wadau mbalimbali walianza kuwa na mawazo ya watoto kuishi kwenye na mazingira ya shule.

Kwa mujibu wa Mwalimu Mgina baada ya kuwa na wazo hilo, wananchi walianza kukusanya mawe na kufyatua tofali kwa ajili ya ujenzi wa hosteli.

“Baadaye vijiji viliibua mradi wa bweni la watoto wa kike na kupeleka maombi ya mradi kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Makete ambaye aliwasilisha ombi hilo TASAF makao makuu,” amesema Mwalimu Mgina.

Amesema maombi yao yalikubaliwa na TASAF ambapo mradi wa kwanza wa ujenzi wa bweni ulianza kujengwa.

“Lakini bado changamoto ziliendelea kuwepo watoto wakiume wakawa wanaendelea kupanga mitaani. Kwa hiyo bweni la wasichana liliwapa hamasa ya kuibua miradi mingine ikiwemo ya ujenzi wa nyumba mbili za walimu,” amesema.

Amefafanua kwamba katika Kata ya Mang’oto kuna vijiji sita, ambapo kijiji kimoja kiliibua mradi wa ujenzi wa nyumba ya walimu (mbili kwa moja) na tayari TASAF imejenga nyumba hiyo na imekamilika.

Aidha, amesema kijiji kingine cha Malembuli kiliibua mradi wa nyumba nyingine ya walimu shuleni hapo ambayo tayari imejengwa na TASAF.

Amefafanua kwamba vijiji vingine viwili vya Isimilo na Mang’oto viliibua mradi wa ujenzi wa bwalo baada ya kubaini wanafunzi wanalia nje chakula nje iwe wakati wa mvua, jua au baridi.

“Kwa kuliona hilo, vijiji viliwekeza nguvu kwa kufyatua tofali, kuandaa mawe, kokoto na maji kuhakikisha bwalo linajengwa, TASAF iliunga mkono kwa kuleta fedha za kununua vifaa vya ujenzi wa bwalo hilo ambapo sasa lilo hatua za mwisho za ukamilishwaji,” alisema na kuongeza;

“Kwa hiyo hii miradi ya TASAF imebadilisha sura ya shule hii na kuwa mpya na hata utoro umefutika, kwani watoto wanaona mazingira ya shule ni mazuri na walimu wana hamasa ya kufanyakazi,” amesema Mwalimu Mgina.

Ameongeza kwamba shule hiyo ni ya mfano kwa TASAF kwa sababu asilimia 75 ya miundombinu ya shule na hivyo kuwa mojawapo ya shule bora kwa wilaya ya Makete.

Diwani wa Kata ya Mang’oto, Osimund Idawa, amesema miradi hiyo ya TASAF iliibuliwa na wananchi kwenye mikutano ya vijiji na baadaye mfuko huo uliwakubalia maombi na kuwapata fedha ambazo imewasaidia kujenga miradi hiyo.

Kwa upande wake Mratibu wa TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Henry Nyigu, alisema kwa mwaka wa fedha 2021/2022 TASAF ilitoa fursa kwa wilaya hiyo kuibua miradi 15.

Kati ya miradi hiyo, alisema 10 ilikuwa ya ujenzi wa miundombinu, ambapo katika Kata ya Mang’oto walibahatika kupata miradi mitano, ambayo ndani yake ipo ya ujenzi wa bweni la wasichana lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80.

Aidha, amesema wakati wa uibuaji wa miradi hiyo, jamii husika ya Kijiji cha Malembuli iliibua mradi huo wa ujenzi wa bweni kupitia mikutano ya kijiji.

Alisema mradi huo ulipitishwa na kuidhinishiwa fedha kwa ajili ya ujenzi.Amesema ambalo watoto wa kike walikuwa wanakaa lilikuwa limechakaa, lenye nyufa kiasi cha kuhatarisha maisha ya wanafunzi.

Amesema wananchi walikubaliana kuchangia vifaa vya ujenzi ikiwemo mawe, tofali, kokoto na nguvu kazi.

Amesema utekelezaji wa maradi huo ulianza 2021 ambapo gharama za ujenzi wa bweni hilo kwa awamu ya kwanza ilikuwa sh. milioni 103 ambazo zinajumuisha fedha za ujenzi na usimamizi.

Aidha, alisema TASAF iliongeza fedha zingine sh. milioni 43 kwa ajili ya ukamilishaji wa mradi baada ya fedha kupelea kidogo.

“Na sasa hivi bweni limekamilika, kila kitu kipo ndani na watoto wataanza kuishi kwenye bweni hilo,” amesema.

Mwonekano wa ujenzi wa bwalo la kulia chakula katika Shule ya Sekondari Mang’oto iliyopo wilayani Makete, mkoani Njombe ambalo linajengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) baada ya mradi huo kuibuliwa na wananchi na wao kuchangia nguvu kazi isiyopungua asilimia 10. Mbali na bwalo TASAF imejega nyumba za walimu nne na bweni lenye uwezo wa kichukua wanafunzi 80 wa shule wa kike. (Picha na mpiga picha wetu)