Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online -Mwanza
JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza linaendelea na msako wa kumtafuta kijana mmoja (jina limehifadhiwa) kwa tuhuma za kumuua Abel Mazuri (25) na kujeruhi watu wawili kufuatia ugomvi uliotokana na ushabiki wa mpira kati ya timu za Simba na Yanga.
Tukio hilo limetokea Machi 24, 2026 majira ya saa 5:30 usiku katika kitongoji cha Nyamahengo, kijiji na kata ya Sumve, wilayani Kwimba mkoani Mwanza.
Inadaiwa kuwa mtuhumiwa alimshambulia marehemu kwa kumchoma kifuani kwa kitu chenye ncha kali akiwa katika banda la kuoneshea mpira, kisha kuwajeruhi watu wengine wawili waliokuwepo eneo hilo wakinywa pombe na kuangalia mchezo.
Akizungumza Machi 25,2026,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbord Mutafungwa,amesema waliojeruhiwa ni Semen Cherehani (26) na Ndubu Chagula (26), wote wakazi wa kijiji cha Sumve, ambao walipata majeraha mikononi. Majeruhi hao wamepatiwa fomu za matibabu (PF3) na wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali Teule ya Sumve, huku hali zao zikielezwa kuimarika.
Mutafungwa amesema,uchunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha tukio hilo ni ubishani uliotokana na ushabiki wa mpira uliovuka mipaka. Polisi wanaendelea na juhudi za kumkamata mtuhumiwa ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Katika tukio jingine, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linafanya uchunguzi na kumsaka mwanamke ambaye hajafahamika anayetuhumiwa kumtupa mtoto mchanga wa kiume mwenye umri wa takribani siku moja.
Mutafungwa amesema,tukio hilo lilitokea Machi 24, 2026 majira ya saa 11:00 jioni katika kitongoji cha Igudija, kijiji cha Kitumba, kata ya Kisesa, wilayani Magu. Mtoto huyo alikutwa ametupwa katika jengo ambalo halijakamilika kujengwa.
Juhudi za kumuokoa mtoto huyo zilifanyika, hata hivyo alifariki dunia kabla ya kufikishwa katika kituo cha afya. Mwili wa mtoto huyo umefanyiwa uchunguzi wa kitaalamu huku taratibu nyingine za kisheria zikiendelea.
Ametoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa watuhumiwa wa matukio hayo. Aidha, limetoa rai kwa jamii kuepuka vitendo vya ukatili na badala yake kutafuta msaada pale wanapokumbana na changamoto za maisha.
“Ninawakumbusha wazazi na jamii kwa ujumla kuwa kutelekeza au kuua watoto ni kosa la jinai na ni kinyume cha haki za binadamu.Ni vyema kutafuta msaada wa kisaikolojia au kijamii kupitia mamlaka husika unapoona changamoto za kulea badala ya kuchukua hatua zinazogharimu maisha ya viumbe wasio na hatia,”amesema Mutafungwa.

More Stories
NMB ilivyosaidia Serikali kukusanya zaidi ya Sh trilioni 9.8
Serikali yaongeza nguvu kwa wachimbaji wadogo,yasisitiza usalama Migodini
REA imeleta mageuzi sekta ya nishati