May 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ACT-Wazalendo yazindua Ilani ya vipaumbele 10

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimezindua Ilani yake ya Uchaguzi Mkuu 2020 yenye vipaumbele muhimu 10 vyenye majibu ya mkwamo na changamoto mbalimbali za Watanzania.

Uzinduzi wa Ilani hiyo ulifanyika jijini Dar es Salaam jana, ambapo Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo alimkabidhi ilani hiyo mgombea urais wa chama hicho, Bernard Membe.

Kupitia Ilani hiyo, ACT-Wazalendo imedhamiria kutekeleza na kuvisimamia vipaumbele hivyo ambavyo ni pamoja na Ujenzi wa Demokrasia na utoaji haki za watu, ufanisi na ubora wa huduma za jamii, uchumi wa watu, uhuru kwa kila mtu, elimu bora ya kivumbuzi bila malipo na kilimo cha kimapinduzi na mazingira wezeshi ya biashara.

Kwa mujibu wa Zitto, vipengele vingine ni usawa na ustawi wa wanawake na vijana, hifadhi ya jamii kwa kila mtu, afya bora kwa wote, ushirika wa kisasa kwa maendeleo jumuishi, Haki za watu wenye ulemavu, maji safi, salama na gharama nafuu na ajira mpya milioni 10.

Akieleza ahadi hizo zitakavyotekelezwa, Zitto alianza kuchambua baadhi ya vipengele vya vipaumbele kama ifuatavyo;

Elimu ya Juu

Amesema chama hicho kitafuta mikopo yote ya miaka ya nyuma iliyotolewa kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kuanza kutekeleza mfumo mpya wa kugharamia elimu ya juu, Serikali italipia Ada ya Masomo (Tuition

Fee), fedha za vitabu (Stationeries), na gharama za mafunzo kwa vitendo (Field Studies/Internship) kwa kila mwanafunzi anayedahiliwa kwenye Chuo Kikuu.

“Wanafunzi watachukua mikopo kwa wanaotaka kwa ajili ya gharama za maisha tu (Meals and Accommodation). Mfumo mpya utaanza Mwaka wa Masomo 2021/2022,” amesema Zitto.

Akieleza jinsi fedha zitakakapotoka, Zitto amesema gharama za elimu ufundi na elimu ya Juu zitatokana na mapato ya Tozo ya kuongeza ujuzi (Skills Development Levy-SDL).

Amesema tozo hiyo itatozwa kutoka waajiri wa sekta binafsi na sekta ya umma kwa kiwango cha asilimia 2 ya gharama za mishahara. “Hivi sasa tozo hii inatozwa kwa sekta binafsi peke yake kwa kiwango cha asilimia nne ya gharama zote kwa wafanyakazi walioajiriwa na kampuni husika ( SDL is charged based on the gross pay of all payments made by the employer to the employees employed by such employer ),” amesema.

Amesema baada ya marekebisho ya kupanua wigo wa walipaji, Serikali itakuwa na uwezo wa kukusanya sh. Bilioni 470 kila Mwaka. Amesema mapato haya yataongezeka kulingana na kuongezeka kwa shughuli za uchumi wa nchi na ajira nyingi zaidi kutengenezwa.

Bima ya Afya kwa Wote

Pia, Zitto amesema kuboresha mfuko wa Bima ya Afya kwa kuunganisha na mifumo ya Hifadhi ya Jamii, ili kila Mtanzania anapochangia hifadhi ya jamii awe anapata huduma ya afya moja kwa moja.

“Kwa mfumo huu, mfuko wa Bima ya Afya utaweza pia kupata fedha kwa wakati na kulipa watoa huduma kwa wakati,” amesema.

Amesema Bima ya Afya ni haki ya kila Mtanzania, itaisimamia kikamilifu haki ya kila Mtanzania kuwa na Bima ya Afya yenye kumpa kinga ya matibabu bila kujali hali yake ya kiafya (wakati wa kujiunga na bima).

Akieleza fedha zitatoka wapi, Zitto amesema kupitia vyama vya Ushirika na vikundi vya uzalishaji vya wananchi hususan wakulima, wafugaji na wavuvi Serikali itaanzisha mfumo wa kuchangia wananchi wanaochangia Skimu ya Hifadhi ya Jamii.

Serikali itatenga fedha kutoka kwenye bajeti kila mwaka kuchangia michango ya wananchi kwenye Hifadhi ya Jamii (matching scheme).

“Kwa mfano katika mchango wa sh. 30,000 kwa mwezi, Serikali itamchangia mwananchi sh. 10,000. Kwa njia hii kila Mtanzania atakuwa na Bima ya Afya Kama Fao katika Skimu ya Hifadhi ya Jamii.

Skimu hii itawezesha Taifa kuwa na Akiba kubwa kwa uwiano wa Pato la Taifa (savings – GDP ratio) na hivyo kuwezesha uwekezaji mkubwa na wa muda mrefu kufanyika,” amesema Zitto.

Aliongeza kuwa kwa makadirio ya watu milioni 6 watakaojiunga na Skimu ya Hifadhi ya Jamii, Mfuko utakuwa na makusanyo ya sh. trilioni 2.2 kwa mwaka, katika hizo, sh. Bilioni 648 zitachangiwa na Serikali kutoka kwenye Bajeti.

Kwa upande wa maji safi na salama kwa kila Mtanzania, Zitto amesema Serikali ya chama hicho itawekeza sh. trilioni 10 ndani ya miaka mitano, wastani wa sh. trilioni 2 kwa kila mwaka, kwenye kumaliza kabisa tatizo la maji safi na salama kwa wananchi.

“Hii ni pamoja na kujenga na kupanua miundombinu ya maji safi pamoja na maji taka,” amesema.

Kuhusu fedha zitatoka wapi, Zitto amesema gharama za ujenzi wa miradi ya maji zitagharamiwa na Tozo Maalumu ya Matumizi ya Mafuta ya Petroli. Serikali itachukua mkopo nafuu wa muda mrefu wa sh. trilioni 10.