May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Muonekano wa kipande cha barabara kinachounganisha Daraja la Nyerere na Kigamboni kikiwa kimekamilika kwa zaidi ya asilimia 99

Kukamilika kipande cha barabara inayounganisha Daraja la Nyerere kwawafurahisha wana-Kigamboni

Na Mwandishi Wetu

BAADHI ya wananchi wa Kigamboni, jijini Dar es Salaam wameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli kupitia Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kukamilisha mradi wa ujenzi wa kipande cha barabara kinachounganisha Daraja la Nyerere na eneo la Kigamboni, ambapo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 99.

Akizungumza kwa niaba ya wakazi wa Kigamboni jana, Godfrey Kurumwa amesema mradi huo wa barabara ni tija kubwa kwa wakazi wa Kigamboni, kwani utafungua fursa za kiuchumi na kijamii hasa ukizingatia mji wa Kigamboni unakuwa kwa kasi kubwa.

“Namshukuru sana Rais (Magufuli) pamoja na NSSF kwa kukamilisha ujenzi wa kipande hiki cha barabara ambayo ni tija kubwa sana kwetu na umependezesha mji wetu,” amesema.

Kurumwa amesema barabara hiyo ni ya kipekee, pana na kwamba imejengwa kwa viwango na ubora wa hali ya juu, ambapo imeleta mandhari nzuri katika mji wa Kigamboni.

Awali, Mhandisi Mkazi Simon Mgani ambaye ni msimamizi wa mradi huo kutoka TANROADS, alimueleza Mkurugenzi Mkuu NSSF, William Erio, aliyetembelea kukagua utekelezaji wa mradi huo jana, kuwa kazi ya ujenzi wa barabara hiyo imekamilika na baada ya siku 14 wataikabidhi rasmi kwa NSSF.

Mhandisi Mgani amesema hivi sasa wanachokifanya ni kuiweka barabara hiyo katika hali ya usalama kwa sababu ni pana, hivyo wanahitaji igawanywe kwa rangi nyeupe na njano ili kutenganisha njia za magari yanayokwenda sehemu mbalimbali.

Amesema kitaalamu rangi haiwezi kupakwa mara baada ya barabara kuwekwa lami kwa sababu inakuwa haijapoa, hivyo inahitaji muda wa kukauka vizuri ambao ni kipindi cha wiki mbili.

Mhandi Mgani amesema Agosti 14, mwaka huu, waliahidi kukamilisha kazi za ujenzi wa barabara hiyo leo, mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, ikiwa ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na Rais Magufuli, Februari 11, mwaka huu, wakati akizindua majengo ya Halmashauri ya Manispaa ya Wilaya ya Kigamboni, ambapo aliagiza mradi huo unao gharimu sh. bilioni 21.39 kukamilika bila nyongeza yoyote.

Amesema kipindi hichi wanaendelea kuwaunganisha wananchi na barabara hiyo kwa kuwawekea makalavati ili waweze kuingia na kutoka majumbani mwao.

Mhandisi Mkazi, Saimon Mgani (wa kwanza kulia) akimuonesha Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, William Erio (wa katikati) pamoja na Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi, Gabriel Silayo wakati hatua iliyofikiwa ukamilishaji wa mradi wa NSSF wa ujenzi wa kipande cha barabara kinachounganisha Daraja la Nyerere Kigamboni. Ujenzi huo umekamilika kwa zaidi ya asilimia 99. Erio alikagua ujenzi huo jana.

Naye, Mkurugenzi Mkuu Erio, amesema lengo la ziara hiyo ni kuangalia ahadi ya mkandarasi anayejenga barabara hiyo ambaye aliahidi kukabidhi kipande hicho cha barabara ya Kibada-Feri kinachounganisha Daraja la Nyerere ambapo alikuta kazi imekamilika.

“Tumekuta mkandarasi kazi ameikamilisha kama alivyosema isipokuwa barabara bado haijawa salama kukabidhiwa kwetu (NSSF),” amesema.

Amesema barabara hiyo haijakabidhiwa moja kwa moja NSSF kwa sababu kubwa mbili; moja ni kwamba mkandarasi amemaliza kuweka lami, na kwa mujibu wa utaratibu inabidi iachwe muda ishindiliwe na sababu ya pili mkandarasi hajaweka alama za barabarani kwani anaisubiri barabara ikauke.

Erio amefafanua kuwa kutokana na sababu hizo mbili, mkandarasi amesema barabara hiyo haitakuwa salama kuanza kutumika kwa sasa, lakini kazi za msingi zimekamilika ambapo itachukua takribani wiki mbili kuikabidhi moja kwa moja NSSF na watu wataanza kuitumia.