March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yajitosa kuratibu safari kuwasaidia waislamu Mwanza kuhiji

Na Daud Magesa, Timesmajira Online-Mwanza

Serikali mkoani Mwanza imelitaka Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza, kuendeleza ushirikiano na taasisi zake kuratibu safari za mahujaji wanaokwenda kuhiji mwaka huu wa 1447 Hijria, huku ikiahidi kusaidia  Waislamu  kuhakikisha wanatimiza nguzo hiyo muhimu ya dini yao.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amiry Mkalipa, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, wakati akifungua kongamano la kitaifa la Hijja lililofanyika jijini Mwanza.

Mkalipa amesema Serikali ipo tayari kushirikiana kwa karibu na BAKWATA kuhakikisha waumini wa dini hiyo wanapata fursa ya kuhiji Makkah mwaka huu.

“Tupo bega kwa bega na taasisi za dini. Tutaratibu safari ya Hijja, tutafahamu idadi ya wanaokwenda na kuunga mkono mahitaji yao ili waweze kushiriki ibada hii tukufu,” amesema Mkalipa.

Pia , serikali katika kongamano hilo, imetoa rai kwa waislamu kuwekeza katika elimu ya watoto wao ikiwemo elimu ya dini, ili kuimarisha msingi wa imani na kumfahamu Mwenyezi Mungu katika hatua za awali za maisha.

“Kama tunataka kizazi kinachomcha Mungu, hatuna budi kuwekeza katika elimu bora. Tuwaandae watoto wetu waifahamu misingi ya dini, waepuke njia za mkato na uongo unaoharibu jamii,” amesisitiza Mkuu huyo wa Wilaya.

Mkalipa amewahimiza masheikh kuandaa semina kila  mara kwa ajili ya  wanaojiandaa kuhiji,watumie jukwaa hilo kuwaelimisha vijana  tofauti ya uchumi halali na haramu, huku akisisitiza umuhimu wa kutenga muda wa kuelezea masuala ya zaka katika makongamano kama hayo.

“Masheikh, vijana wetu wanaotafuta uchumi wanahitaji maarifa ya kiuchumi kwa mujibu wa dini. Msiwaache waendelee kwenye biashara zisizo halali kwa kukosa uelewa. Elimisheni, fundisheni misingi halali na haramu,” amesema.

Aidha, amewahimiza viongozi wa dini kuwekeza katika ardhi kwa  maendeleo ya Waislamu; “Ardhi ya bei nafuu inaisha. Nunueni  kwa wakati huu na kuiweka chini ya BAKWATA kwa ajili ya vizazi vijavyo.”

Naye  Mjumbe wa Baraza la Ulamaa Zanzibar, Sheikh Suweid Ali Suweid,ameeleza kuwa, Hijja ni wajibu wa kila Muislamu mwenye  uwezo kwani  kuna umuhimu wa kuwasaidia  wasio na uwezo ili watimize ibada hiyo.

“Tushirikiane kwa mambo ya kheri,tukatae dhana ya kuwa sisi ni masikini wa milele. Mwanza ina watu zaidi ya milioni 3,ni wakati sasa watu 400,000 waruke kwa ndege kwenda kuhiji,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Sheikh Othman Hamis Juma akiwasilisha mada kuhusu “Dhana ya Uwezo wa Kwenda Hijja”, akifafanua kuwa kila mtu ana uwezo wa kuhiji endapo ataweka mipango sahihi na kumtegemea Mwenyezi Mungu.

“Mwenyezi Mungu ana neema nyingi zisizopimika, lakini haziji bila utaratibu na kutamani pekee hakutoshi, lazima kuwe na matumaini na maamuzi. Jisogezeni kwa Mungu kwa Sunna, atawapa uwezo,” amesema Sheikh Othman.

Akitoa salamu za BAKWATA, Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke, amesema kongamano hilo ni muhimu kwa  elimu, kushirikishana maarifa na kuhimiza mshikamano wa kidini miongoni mwa Waislamu.

“Mwaka huu wa 1447 Hijria, tunatarajia kuona idadi kubwa ya Waislamu wa Mwanza wakitimiza ibada ya Hijja, si tu kwa uwezo wa kifedha bali  maandalizi, mipango na mshikamano wa dhati,” amesema.