Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KAMPUNI ya Bia ya Tanzania (TBL) imekutana na wakulima wa shayiri Monduli Juu, mkoani Arusha kwa ajili ya kuwapatia mafunzo ya vitendo na ushauri wa kitaalamu wenye lengo la kuongeza mavuno na kuboresha ubora wa zao hilo ili kuleta tija katika mnyororo wa thamani wa kilimo nchini.
Mafunzo hayo yamefanyika wakati wa Siku ya Wakulima wa Shayiri, hafla iliyoongozwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Monduli, Mheshimiwa Muhsin Kassim, na kuhudhuriwa na wakulima zaidi ya 200, viongozi wa jamii na wadau wa sekta ya kilimo. Tukio hilo limekuwa jukwaa la kubadilishana maarifa na kujadili suluhu za kufanikisha ukuaji endelevu wa kilimo cha shayiri.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kassim amesema serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya kuongeza tija kwa wakulima kupitia upatikanaji wa pembejeo, huduma bora za ugani na upanuzi wa masoko ya mazao. “Wakulima ndiyo uti wa mgongo wa taifa letu. Leo tunasherekea kazi zao na kuthibitisha upya dhamira ya kuwasaidia kupitia utafiti, huduma za ugani na masoko yenye tija,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masuala ya Sheria na Mahusiano ya Kampuni wa TBL, Neema Temba, amesisitiza dhamira ya kampuni kuendelea kununua shayiri kutoka kwa wakulima wa ndani na kuwawezesha kupitia ushiriki shirikishi wa kiuchumi. “TBL tumejikita katika kuimarisha uhusiano na wakulima na kuunga mkono kilimo endelevu kinachowanufaisha wote katika mnyororo wa thamani,” amesema.

Hafla hiyo ilihusisha Shamba Darasa na vipindi vya kubadilishana maarifa, pamoja na majadiliano kuhusu changamoto za kilimo cha shayiri ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, upotevu wa mazao baada ya mavuno na upatikanaji wa pembejeo bora.

Siku ya Wakulima wa Shayiri ilihitimishwa kwa wito wa pamoja wa kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi, wakulima na taasisi za serikali ili kuongeza tija, uendelevu na upatikanaji wa masoko ya shayiri nchini.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi