November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TASAF yajipanga kutekeleza miradi kwa ufanisi

Na Patrick Mabula, TimesMajira Online, Dodoma

MKURUGENZI Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Ladislaus Mwamanga amesema wamejipanga ipasavyo katika kutekelezaji wa mradi wa awamu ya tatu wa kutoa fedha za ruzuku za kunusuru kaya masikini unaotarajiwa kuanza mara baada ya kukamilika kwa zoezi la kubainisha walengwa.

Tayari TASAF III katika utekelezaji wa mradi huo wa kupambana na umasikini awamu wa tatu, imeshazishughulikia changamoto zilizokuwepo katika utekelezaji wa awamu ya kwanza na ya pili nhivyo watahakikisha mapugufu hayo hayajitokezi tena hasa kuhusu fedha zitakazotolewa kwa walengwa watakaokuwa wamebainishwa.

Amesema, katika utekelezaji wa TASAF III watafuatilia kwa karibu zaidi changamoto kwa walengwa ambao ni kaya maskini zinazoishi kwenye mazingira duni ambazo zitakuwa zikipatiwa ruzuku ya fedha za serikali .

“Serikali katika mpango wa kunusuru kaya maskini imeamua kuanzisha awamu ya tatu ya (TASAF III ) ambao unahusisha Halmashauri 159 za Tanzania Bara na Zanzibar lengo likiwa kuziwezesha kaya hizo maskini kujiongezea kipato pamoja na kuweza kugaharamia mahitaji mbalimbali muhimu, ” amesema Mwamanga

Mkurugenzi wa progaramu za jamii, Amadeus Kamagenge amesema, katika utekelezaji wa mpango wa TASAF III, jambo muhimu kwa walengwa watakaokuwa wameandikishwa ni pamoja na kupima uwezo wa kufanya kazi ambao kitakuwa kipaumbele katika kuwapatia fedha za ruzuku.

Kamagenge amesema, katika utekelezaji wa mradi wa TASAF nchi nzima, changamoto zote zitakazokuwa zinajitokeza watakuwa wanazifanyia kazi haraka sana kwa faida ya walengwa.

Awali mgeni rasmi alipokuwa akifungua kikao kazi cha kuwajengea uelewa waandishi wa habari kuhusu mradi wa TASAF III, kutoka Mikoa ya Singida, Dodoma, Iringa na Shinyanga, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Maduka Kessy amesema, vyombo vya habari vina nguvu na ushawishi mkubwa kwa jamii katika kupambana na umasikini na kuleta matokeo chanya.

Kessy amesema, kila Mtanzania ana nafasi katika kuchangia na kuinua pato la Taifa ili twende mbele zaidi hivyo waandishi wa habari kwa taaluma yao wanadhamana kubwa ya kuelimisha na kuhamasisha wananchi wa kipato cha chini ambao ndiyo welengwa kufanya kazi kwa bidii na kupiga vita umaskini .

Mtaalamu wa ufatiliaji na tathimini wa TASAF, Faraj Mishael amesema, taarifa ya Benki ya Dunia kuhusu hali ya umasikini inaonyesha bila kuwepo kwa TASAF umaskini Tanzania ungeongezeka kwa asilimia mbili (2) na umaskini uliokithiri ungeongezeka kwa asilimia nane hadi 9.2 hivyo wanahabari wana jukumu kubwa la kuielimisha jamii ili umaskini uweze kupungua zaidi.

Kwa upande wake, mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TASAF, Zuhura Mdungi amewataka wahabari kutoa taarifa za ukweli kwa umma zenye usahihi na kwa wakati katika kipindi cha pili cha mradi wa awamu ya tatu ambazo zitasaidia kufikia malengo mahususi ya serikali kwa nguvu ya pamoja zitakazowajengea imani wananchi kuwa wanaweza kuondokana na umaskini na kuweza kuchangia pato la Taifa.