Na Mwandishi Wetu,Morogoro
WAKATI kipyenga cha uchukuaji fomu kwa wagombea wa nafasi mbalimbali ikiwemo Urais, Ubunge na Udiwani kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya kuwapata wagombea wa kupeperusha bendera ya chama hicho kikiwa bado hata hakijapulizwa tayari michezo michafu ya inayohusishwa na rushwa imedaiwa kuanza katika jimbo la Uchaguzi la Morogoro Mjini.
Hatua hiyo imedaiwa kuwahusisha makatibu wa kata 27 kati ya 29 zilizopo katika jimbo hilo ambapo mchakato huo unadaiwa kufanywa kwa usaidizi wa Katibu wa CCM wa Wilaya ya Morogoro Mjini Twalib Bellege kwa lengo la kumbeba Mbunge aliyepo madarakani Abdulaziz Mohamed Abood.
Kupitia kikao Cha Makatibu hao wa kata kilichoitishwa na Katibu wa Wilaya Juni 7, mwaka huu kikiwa na ajenda saba, pamoja na mambo mengine kilitoa maagizo kwa Makatibu hao kutumia nafasi walizonazo kumpigia ‘debe’ Abood aweze kupita katika kura za maoni ili aweze kugombea tena nafasi hiyo ya Ubunge katika uchaguzi ujao.
” Tulipewa maagizo mbalimbali ambayo kimsingi mengine ya kiutendaji ikiwemo kuzingatia taratibu za ujazaji wa majina kwa kufuata alfabeti katika fomu za kuomba kuteuliwa ambayo tuliyapokea kama ilivyotakiwa, tofauti na hayo ni maagizo ya kuhakikisha tuhakikishe jina la Mheshimiwa Abood tunalipigania ili aweze kupita” alisema mmoja wa wajumbe aliyehudhuria kikao hicho
Alisema kikao hicho kilichofanyika katika Ofisi ya CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, kiliwahusisha wajumbe kutoka Kata 27 kati ya Kata 29 zilizopo katika Wilaya hiyo Morogoro Mjini huku wakielezwa kuwa vikao vingine kama hivyo na vingine vya muendelezo wa mikakati hiyo vikipangwa kufanyika mbeleni.
” Tuliambiwa kuwa vikao hivyo ni vya siri na sote tulioidhuria hatupaswi kuvujisha siri hiyo kwa makubaliano maalumu, baada ya sisi na Katibu huyo wa Wilaya kukubaliana , aliwasiliana na mhusika na baada ya muda mfupi ndugu wa Abood aitwaye Ally alikuja na bahasha mbili zenye fedha, moja kwa ajili yetu Makatibu wa Wilaya na bahasha nyingine kwa ajili ya viongozi wa Wilaya” aliongeza
Alisema kila kwa upande wa kila mjumbe kutoka ngazi ya Kata alipewa bahasha yake yenye kiasi Cha Sh 100,000 huku wakielezwa kuwa huo ni mwanzo na kwamba kadri watakavyokuwa wakiitwa au kukutana katika vikao vingine watapewa zaidi.
” Kwa sisi tunaopenda haki na kuepuka kukichafua Chama chetu ambacho kimejipambanua kusimamia haki Kwa kila mgombea jambo hili hatukuliona kama linapaswa kufumbiwa macho lakini huwezi kusema mbele ya wajumbe wenzako kwa kuwa ungeonekana kuwa msaliti” ameongeza mtoa taarifa huyo ambaye jina lake limehifadhiwa
Alisema huo ni mkakati wa Mbunge huyo ambaye ametoa maagizo kwa Katibu wa CCM wa Wilaya kumuandalia vikao hivyo ili kumrahisishia kukutana na kundi la wajumbe hao kwa pamoja badala ya kutembea hadi ngazi za Kata kitu ambacho amedai kuwa hakijawahi kufanywa na Mbunge huyo kwa madai kuwa hana utaratibu wa kushuka chini.
Alidai kuwa hiyo sio mara ya kwanza kufanyika michezo michafu ya Kisiasa wilayani humo kufanyika chini ya Katibu huyo wa Wilaya kwani kwani hapo awali kwa maelekezo ya Mbunge, aliwahi kuitisha kikao cha haraka haraka cha wenyeviti wa Serikali za Mitaa kwa kisingizio kuwa ni semina, ilipojulikana kuwa wevyeviti na Mabalozi watapiga kura za maoni ndani ya Chama ambapo mbunge huyo alitoa fedha sh 30,000 na t-shirt yenye kujifanyia kampeni kwa kila mshiriki.
Kwa upande wake Mjumbe mwingine ambaye kama alivyo kwa Mjumbe wa kwanza amedai kuwa mtengenezaji wa mazingira yote ya Mbunge huyo ni huyo Katibu wa CCM Wilaya akisisitiza kuwa kuna mambo mengi amefanya kwa lengo la kumbeba katika nafasi hiyo na vikao vingine vya Chama.
Aidha ameziomba mamlaka ambazo zinahusika na uchunguzi kuifanyia kazi suala hilo kwa madai kuwa kama halitoshughulikiwa linaweza kubaribu mchakato wa uchaguzi unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Akijibu tuhuma hizo Katibu huyo wa CCM Wilaya ya Morogoro Twalib Berege alikana kugawa fedha hizo kwa wajumbe hao huku akisisitiza kuwa kwa Kipindi hiki tuhuma na malalamiko kama hayo ni kawaida kutokea.
“Ajenda ya kikao ilikuwa moja tu kuhusu maandalizi ya Uchaguzi, huyo aliyesema kuwa tuligawa fedha basi akuthibitishie lakini hata kama kweli huyo anayetajwa kutoa fedha angefanya hivyo ndani ya Chama haina tatizo kwa kuwa yupo madarakani anakisaidia Chama”
“Kwanza Mbunge mwenyewe kwa sasa yupo nje ya nchi, angewezaje kuja katika kikao na kutoa fedha hizo” alisema Katibu huyo na hata alipoambiwa kuwa aliyetumwa kuleta fedha hizo ni ndugu wa Mbunge huyo alisisitiza kuwa hakuna kitu kama hicho.
Alipotafutwa Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya hiyo ya Morogoro ili kupata ufafanuzi wa suala hilo, aligoma kutoa ushirikiano akidai kutokuwa na taarifa yoyote juu ya kufanyika kwa kikao hicho na badala yake akashauri atafutwe Katibu Mwenyewe.
Mbunge Abdulaziz Mohamed Abood ili kuzungumzia suala hilo simu yake haikuweza kupatikana pengine ni kutokana kuwa safarini nje ya nchi kama ilivyoelezwa na Katibu huyo wa CCM wa Wilaya ya Morogoro.
More Stories
Ussi awataka wananchi Handeni kulinda miundombinu ya maji
Daraja la J.P.Magufuli kuzinduliwa Juni 19,2025
Yas yazidi kuboresha huduma sekta ya Utalii