December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jaji Warioba: Viongozi wamegeuka watoa rushwa

Na Rose Itono

WAZIRI Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema pamoja na Serikali za awamu zote kupambana na rushwa, lakini tatizo hilo bado ni kubwa kwa viongozi na hali ni mbaya.

Ameongeza kuwa Rais John Magufuli anahitaji msaada mkubwa kupambana na vitendo hivyo, kwani hali ya rushwa sasa imebadilika na viongozi ndiyo wanatoa rushwa badala ya wao kupokea rushwa.

Akizungumza kwenye Kongamano la Maadhimisho ya Kumbukizi ya Mwalimu Julius Nyerere lililoandaliwa na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) jana jijini Dar es Salaam, Jaji Warioba alisema ni ukweli kuwa rushwa imekuwa ikisimamiwa zaidi kwa wafanyabiashara na wananchi, lakini ni wazi kwa upande wa viongozi hali bado ni mbaya.

“Rais Magufuli ana ajenda madhubuti za kumuunga mkono Nyerere kwenye suala zima la uadilifu, mapambano y rushwa kwa lengo la kulinda uadilifu kwa taifa, lakini anahitaji msaada kwani rushwa imebadilika sasa hivi viongozi hawapokei rushwa badala yake wao ndiyo wanatoa,”alisema Warioba.

Alishauri ili vita hiyo iweze kufanikiwa TAKUKURU isiingiliwe na kiongozi yeyote zaidi ya Rais ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi.

Aidha, alitoa mfano akisema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa mwaka huu rushwa imetumika kwa viongozi ambao ni wajumbe kwenye zoezi la upigaji kura kwa ajili ya kuchagua wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi.

“Hiki ni kipindi cha kuelekea uchaguzi vyama vyote vilijadiana kuachana na tabia ya vitendo vya rushwa na mfano mzuri tumeuona kwa wajumbe kwenye mchakato wa kura za maoni,”alisema Jaji Warioba.

Pia alisema hatuwezi kuimaliza rushwa hadi wananchi wajifunze kuikataa na viongozi waache kutoa.

“Viongozi wote kwa pamoja waje na azimio jipya ambalo litamaliza vitendo hivyo,”alisema Jaji Warioba

Kwa upande wake Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Temeke, Donasian Kessy akitoa mada kuhusu falsafa ya Mwalimu Nyerere katika mapambano dhidi ya rushwa, alisema rushwa ni zao la uozo wa kina ambao unamsukuma mtu kufanya jambo la uhalifu pia ni adui wa haki na maendeleo ya ustawi wa jamii.

Aliwaasa wananchi kuchagua viongozi wasiopenda rushwa ili kulinda utu, kwani hata mtindo wa maisha wa sasa unachangia suala hilo kuwa gumu, kwani wamekuwa wakipenda kuishi maisha ya juu tofauti na vipato vyao.

Kessy aliongeza kuwa vitendo vya rushwa vinasababisha Serikali kushindwa kutoza kodi kwani walipa kodi wengi ni wafanyabiashara na hivyo kusababisha Serikali kushindwa kujiongoza.

Mchangiaji mwingine wa mada ya madhara ya rushwa katika maendeleo ya jamii na utawala bora Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha CAG Mstaafu, Ludovick Utouh, alisema Watanzania wamekuwa wakichukulia kipindi cha uchaguzi kuwa ni cha mavuno.