October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kanali Mtambi aipongeza Klabu ya waandishi wa habari Mara kwa uanzishaji wa Tuzo

Na Raphael Okello, Musoma.

MKUU wa mkoa wa Mara, Kanali Evance Mtambi ameipongeza Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Mara kuanzisha tuzo kwa waandishi wa habari mkoa wa Mara watakaoandika habari bora zenye kuleta matokeo bora kwa jamii.

Kanali Mtambi amesema hayo leo wakati akifungua mdahalo wa “Mara Bora kwa uwekezaji na kuishi” ulioandaliwa na Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Mara(MRPC) na kushirikisha wadau wa maendeleo mkoani humo.

Amesema mpango huo wa kuanzisha tuzo utawafanya waandishi wa habari ndani ya mkoa huo kuongezeza juhudi za uandishi bora katika kutangaza rasilimali zilizoko Mara.

Ametaja baadhi ya rasilimali na vivutio ndani ya mkoa huo.kuwa ni pamoja na makumbusho ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, hifadhi ya taifa ya Serengeti na mapori ya akiba ya Grumet na Ikorongo.

Vivutio vingine ni Ziwa Victoria, madini, kilimo na mifugo na kwamba zikitangazwa vyema mkoa wa Mara utakuwa sehemu salama kwa uwekezJi na kuishi.

“Niwaombe waandishi wa habari mkoani hapa, wadau wa maendeleo na watendaji wa serikali kuhakikisha kuwa wanatangaza vyema fursa za uwekezaji kwa wananchi ndani ya mkoa na duniani kwa ujumla”.amesema.

“Nipongeze Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Mara kuja na wazo hili la mdahalo wa leo pamoja na wazo la kuanzisha tuzo kwa waandishi wa habari ” amesema Kanali Mtambi.

Akitoa maneno ya utangulizi , Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Mara(MRPC), Mugini Jacob amesema lengo la mdahalo huo ni kujadili na kuona namna gani waandishi wa habari wanaweza kuchangia katika kutangaza fursa za uwekezaji bora na mazingira bora ya kuishi.

Mugini amesema katika kuhakikisha kuwa fursa za uwekezaji zinatangazwa, klabu hiyo imeanzisha tuzo kwa waandishi wa habari mkoa humo watakaotangaza na kuandika habari bora katika vyombo mbalimbali vya habari.

Ametaja habari hizo zitakazoanza kutolewa tuzo ndani ya mwaka huu ni zile zitakazohusu madini, utalii, uhifadhi, kilimo, mifugo, biashara, ukatili wa kijinsia na uvuvi.

Baadhi ya wadau wa maendeleo wakichangia hoja katika mdahalo huo wamewataka waandishi wa habari kuwasaidia katika kutangaza shughuli za uwekezaji na fursa mbalimbali na kuepusha taarifa zinazoweza kuwafukuza wawekezaji.