September 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jinsia na ustawi vipengele muhimu kufanikisha maendeleo endelevu

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Riziki Pembe Juma amesema  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua  kuwa Jinsia na Usawa ni vipengele muhimu vya kufanikisha maendeleo endelevu nchini.

Riziki amesema hayo wakati akifunga kongamano la vijana wanawake viongozi  kutoka nchi 16 Baraza Afrika, lililofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimi Nyerere  Kibaha,Mkoa wa Pwani.                                            

Amesema masuala ya jinsia na usawa yameainishwa katika Katiba zote mbili, katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na ya Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar ya mwaka 1984.                                                                                   

Ameeleza kwamba  lengo la kuainishwa humo ni katika kusimamia haki na usawa na kuhimiza ushiriki wa wanawake katika kufanya maamuzi.                                                                                                 

Pia amesema  katika Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2025 imeainsha umuhimu wa Jinsia na Usawa.                                                                                                                   

Amesema katika kufanisha maendeleo hayo Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, na Makundi Maalum (SMT) na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (SMZ) zimeanzishwa kisheria kwa lengo la kuratibu na kusimamia masuala ya Jinsia nchini.

Aidha amesema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaamini kuwa elimu ni moja ya silaha muhimu hasa kwa wanawake ikiwa watakua na nia ya kufikia maendeleo ya  kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Ameeleza kwamba Serikali imeweka makusudi hatua za kukuza elimu ya wasichana na kuwahimiza  waendele kusoma ili wapate elimu ambapo Jamii kwa ujumla inawasaidia wasichana kuendelea na masomo badala ya kuwalazimisha kuingia kwenye ndoa za mapema.

Riziki alitoa wito kwa washiriki wa kongamano hilo kutumia jukwaa hilo kama fursa ya  kujifunza mbinu bora zaidi ambazo zitafanya kuongeza uwezo wao na ujuzi.                   

Amefahamisha kwamba hatua hiyo itasaidia katika  bara la Afrika kuhimiza vijana wa kike kuthamini elimu itakayowasaidia kupata mapato yao na kupata nafasi katika vyombo vya maamuzi.

Kongamano hilo la siku tatu  limehudhuriwa na watu 100
wanawake vijana ambao ni wanachama wa harakati pamoja na Maafisa wa zamani na wanaharakati wanaoendesha mashirika ya wanawake yenye mafanikio kutoka nchi mbalimbali.