November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuanzisha kanzi data ya makundi adimu ya Damu

Na Mwandishi wetu,Dar es Salaam

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema Serikali inadhamiria kuanzisha Kanzi Data ya kutambua makundi ya Damu kwa Watanzania wote, ili kusaidia kukabiliana na Changamoto ya Upatikanaji wa Damu Salama kwa Watu wenye Makundi Adimu ya Damu.

Kwa Mujibu wa Ripoti iliyotolewa na Mpango wa Taifa wa Damu Salama kwa Waziri wa Afya Ummy kwamba inayo kanzi Data ya Watu takribani 350 ambao wapo kwenye Kundi O-Negative baada ya Kuwatambua kama Kundi Adimu la Damu.

Waziri Ummy ametoa kauli hiyo leo Aprili 11, 2023 Jijini Dar es Salaam wakati alipofanya ziara katika Ofisi za mpango wa Taifa wa Damu Salama ili kukagua na kuangalia hali ya Upatikanaji wa damu hapa nchini.

Waziri Ummy pia amepongeza hatua ya Watu takribani Elfu Ishirini (20,032) ambao walijitokeza Kuchangia Damu katika Kipindi cha Wiki ya Matendo ya Huruma kwa Waumini wa Kanisa la Waadventista wa Sabato, Kampeni ya Kitaifa ya Robo Mwaka ya Tatu na Sikukuu ya Pasaka.

Pia ameipongeza Timu ya Yanga kwa kufanikisha ukusanyaji wa damu takribani chupa 544 kwa siku moja

“Nitumie fursa hii kuwapongeza ambao wamekuwa na utaratibu wa kuchangia Damu mara kwa mara ikiwemo kundi lililojitokeza kuchangia damu katika Kipindi hiki cha Sikukuu ya Pasaka” amesema Waziri Ummy.

Katika hatua nyingine Waziri Ummy amekemea tabia ya baadhi ya Watumishi katika Sekta ya Afya kuwauzia Damu wananchi.

Kwa upande wake Meneja wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama Dkt Abdu Juma amemueleza Waziri Ummy baadhi ya Changamoto zinazokabili Mpango wa Taifa wa Damu Salama ikiwemo ile ya Ukosefu wa Magari ya Kukusanyia Damu pamoja na vichomea Taka.