May 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Mpango mgeni rasmi kikao kazi cha tathimini utendaji wa mahakama

Na Daud Magesa, TimesMajira Online Mwanza

MAKAMU wa Rais Dkt. Philip Mpango,kesho Aprili 12,2023 anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye kikao kazi cha tathimini ya utendaji wa mhimili wa Mahakama ya Tanzania kwa kipindi kilichopita.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,Wilbert Chuma akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu Kikao Kazi cha Tathmini ya Mahakama kitakachofanyika Malaika Hoteli kesho,kitafunguliwa na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango na kulia ni Naibu Msajili na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho Mahakama ya Tanzania, Dkt. Angelo Rumisha.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza,leo Aprili 11, mwaka huu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,Wilbert Chuma,amesema kikao kazi hicho ni cha tathimini ya utendaji kazi wa Mahakama ya Tanzania wa mwaka 2022 na mapitio ya mpango kazi wa Mahakama wa 2021 hadi 2025.

Amesema kikao hicho cha siku tatu kitafunguliwa na Makamu wa Rais Dkt.Mpango, kitahusisha mada mbalimbali kikiwa ni pamoja na taarifa ya utendaji kazi wa mahakama kwa mwaka uliopita pia maboresho yaliyofanyika ya mahakama.

“Kutakuwa na mwongozo wa utambuzi wa shughuli za mahakama,pia mada ya utamaduni wa mahakama ikiwemo ya mfumo wa usimamizi wa mashauri ulioboreshwa (Advanced Case Menegment,”amesema Chuma na kuongeza

“Baada ya kikao hicho mtapata fursa pia ya kuelewezwa kwa kina nini kimezungumzwa na kimefanyika ili mpate kwa undani kwa nini hasa,kama mahakama tuna utaratibu wetu wa namna gani ya kuendelea kuhakikisha huduma zetu tunapata muda wa kutathmini nini tumefanya na tunapaswa kuendelea kufanya nini kwa faida na maslahi ya umma.”

Kwa upande wake,Naibu Msajili na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho Mahakama Kuu,Dkt.Angelo Rumisha,amesema mahakama ilifanya maboresho tangu mwaka 2015 ikilenga kupunguza siku za mashauri kukaa mahakamani kuongeza imani kwa wananchi kupitia mahakama.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Profesa Elisante Ole Gabriel, akisistiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo) pichani leo kuhusu na mafanikio ya mhimili huo kuelekea kikao kazi cha tathmini ya utendaji wa mahakama.Kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama hiyo Wilbert Chuma , kushoto ni Naibu Msajili na Mkuu wa Kitengo cha Mahakama, Dkt. Angelo Rumisha.

Amesema mambo wanayofanya lazima yawe na mpango mkakati wa kuwaonesha ni wapi wamefanya,wakati gani na wanatakiwa kufanya nini ambapo baada ya mpango mkakati huo walio nao sasa wana ushirikiano mzuri na Benki ya Dunia (WB)ambayo imetoa fedha kwa serikali ili kufanya maboresho ya mhimili huo.

Dkt.Rumisha amesema maboresho hayo yanalenga mambo manne wanayofanyia kazi ya ushirikishwaji wa wananchi,upatikanaji wa huduma za mahakama,uwazi na uwajibikaji.

“Majaji wanapokutana leo ni kutafakari kuhusu hayo maneneo manne kuwa tumefanya nini na tunatakiwa twende wapi,kitu kikubwa ambacho ni dhahiri kinafanyika ni ujenzi miundombinu ya kisasa ya vituo jumuishi vya utoaji haki vyenye huduma zote jengo moja na wadau wote,vinatumia zaidi TEHAMA katika ubinifu wa utoaji haki,”amesema.

Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,Profesa Elisante Ole Gabriel,amesema mafanikio makubwa ndani ya mahakama wameboresha sana ushirikishwaji wa watumishi katika kupanga mipango mikakati ya utendaji na kurahisisha utekelezaji.

“Serikali inashirikiana na mhimili wa Mahakama na Bunge katika kufanikisha maboresho hayo ambayo tutayazungumzia kwenye kikao kazi,nitoe wito wananchi waendelee kuamimini na kutumia huduma za mahakama pia vyombo vya habari viendelee kuhabarisha umma kwa weledi bila kuwakanganya,”.