November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tuzo za ubora kitaifa zazinduliwa rasmi

Na Doreen Aloyce, TimesMajira Online, Dodoma

WATANZANIA wametakiwa kuchangamkia fursa ya kuwania Tuzo za Ubora za Kitaifa kwa mwaka 2022/2023 ambazo zinahusisha Sekta mbalimbali na watu binafsi wanaofanya vizuri kwenye masuala ya Ubora ambazo zitasaidia kuitangaza nchi.

Akizungumza na Vyombo vya Habari Jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Tuzo za tatu za Ubora za Kitaifa Mwaka 2022/2023 Kaimu katibu mkuu wizara ya uwekezaji, Viwanda na Biashara Aristides Mbwasi amesema kuwa tuzo hizo zitaleta fursa ukuaji na maendeleo ya sekta ya viwanda na Biashara.

Amesema mashindano ya Tuzo hizo ni pamoja na Tuzo kwa kampuni bora , tuzo kwa bidhaa bora , tuzo kwa huduma bora , tuzo kwa muuzaji bora wa bidhaa nje ya nchi na mtu mmoja aliyefanya vizuri kwenye masusla ya ubora .

Pia amesema mashindano hayo wadau watapata fursa ya kufahamika zaidi kwenye jamii na kushiriki kwenye mashindano ya tuzo za ubora kwa jumuia ya Afrika Mashariki , mashundano ya tuzo za ubora kwa nchi za jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika na kufahamika kupata masoko zaidi.

“Serikali kupitia wizara ya uwekezaji ,viwanda na Biashara iliona umuhimu wa kuanzisha tuzo hizi na kutoa jukumu la kuziratibu kwa shirika la viwango Tanzania (TBS) kwa kushirikiana na sekta binafsi nchini (TPSF) Taasisi ya viwango Zanzibar , shirikisho la wenye viwanda nchini ,”

” Pia tumeshirikiana na Shirika la kuhudumia viwanda vidogo nchini (SIDO) ,chama cha wanawake wafanyabiashara Tanzania , Chemba ya Biashara , viwanda na Kilimo Tanzania na mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania “amesema Mbwasi.

Hata hivyo amewataka watanzania kuwa mabalozi wa Kuhamasisha wazalishaji wa Bidhaa na watoa huduma kushiriki mashindano ya Tuzo za ubora za mwaka 2022/2023.

Nae Mkurugenzi mkuu wa shirika la Viwango Tanzania Daktari Athuman Ngenya akizungumzia maandalizi yalivyo mpaka amesema kuwa yanaendelea vizuri kwa kutumia warsha mbalimbali na vyombo vya habari ,mitandao ya kijamii ambapo yatasaidia kuwapata washindi.

“Katika maandalizi haya tumewapa kipaumbele akina mama wajasiliamali kuwahamasisha ili waweze kushiriki kwani ni wengi ambao wamejikita kwenye ujasiliamali.” Amesema Ngenya.

Kwa upande wake Hafsa Ali Slim Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Viwango ambapo akimuwakilisha Mkurugenzi ZBS amesema kuwa wanatarajia kutoa uelewa kwa wafanyabiashara na wazalishaji wa bidhaa mbalimbali kwa upande wa Zanzibar ili waweze kushiriki kwa wingi zaidi.