May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madiwani Manispaa Shinyanga waridhishwa na utendaji kazi wa Rais Samia

Na Suleiman Abeid, Timesmajira Online Shinyanga

MADIWANI katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga wameelezea kuridhishwa na kasi ya utendaji kazi wa Rais Samia Suluhu Hassan hasa upande wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi huku wilaya ya Shinyanga ikiwa imepatiwa zaidi ya shilingi bilioni 11 za miradi ya maendeleo.

Hali hiyo imebainishwa na madiwani hao katika kikao chao cha kawaida cha Baraza ambapo wamesema kitendo cha Rais Samia kusukuma fedha nyingi za maendeleo katika halmashauri zote nchini kimechangia utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo kukamilika kwa wakati.

Madiwani hao wamesema wana kila sababu ya kumpongeza na kumshukuru Rais Samia kutokana na utendaji wake wa kazi ambapo ndani ya kipindi kifupi cha uongozi wake changamoto nyingi za wananchi katika Manispaa ya Shinyanga zimepatiwa utatuzi.

Mariamu Nyangaka ambaye ni diwani wa kata ya Kitangiri amesema hivi sasa wananchi katika kata yake wameonesha kuridhishwa na utendaji wa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na wanamuunga mkono kwa dhati.

“Mheshimiwa mstahiki Meya, kwa niaba ya wananchi wa kata ya Kitangiri nichukue fursa hii kumpongeza Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anazozifanya hivi sasa katika kuhakikisha anawaletea watanzania maendeleo ya kweli waliyoahidiwa,”

“Ndani ya kipindi kifupi cha uongozi wake kata yetu imepokea mamilioni ya shilingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo za hivi karibuni za ujenzi wa vyumba vine vya madarasa katika shule yetu ya Sekondari, tunamshukuru na tunampongeza kwa dhati,” ameeleza Nyangaka.

Nyangaka amesema hivi sasa Serikali inaendelea kutatua changamoto zilizokuwepo kwenye kata yake kila kunapokucha, na kuwezesha kupungua kwa kiasi kikubwa kwa changamoto na badala yake mafanikio katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndiyo yanayoonekana.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Shinyanga mjini, Arnold Makombe aliyekuwa miongoni mwa wageni waalikwa kwenye kikao hicho, amesema CCM kwa sasa inaridhishwa na utendaji wake ndani ya Serikali katika suala zima la utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho.

“Nichukue nafasi hii kukupongezeni viongozi na watendaji wote ndani ya Manispaa yetu ya Shinyanga, kwa kweli sisi CCM tunaridhishwa na kasi ya utendaji wenu wa kazi kwa hivi sasa, niseme tu kwamba tunachohitaji ni ushirikiano wa pamoja, tunawashukuru kwa kazi nzuri zinazofanyika,”

“Kazi zinazofanyika hivi sasa itaturahisishia sisi kipindi cha kampeni kwenye chaguzi zijazo za mwaka 2024 na 2025, kazi yetu itakuwa rahisi, maana mambo mengi tuliyowaahidi wananchi yatakuwa yametekelezwa hivyo hawatakuwa na shaka tena na Serikali ya CCM,” ameeleza Makombe.

Pamoja na pongezi za madiwani hao pia wameomba changamoto ndogo ndogo zilizopo kwenye kata zao kwa hivi sasa ni vyema zikafanyiwa kazi ikiwemo kuongeza matundu ya vyoo katika shule za msingi na sekondari ambazo bado zina uhaba wa matundu ya vyoo na vyumba vya madarasa.

Kaimu mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Getruda Gisema amesema tayari Manispaa yake imejipanga kumaliza changamoto zote zilizopo kwenye kata hasa upande wa ujenzi wa matundu ya vyoo na vyumba vya madarasa ili kuweza kukidhi mahitaji yanayohitajika.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Elias Masumbuko amewaomba madiwani wahakikishe muda wote wanazingatia kanuni za Manispaa kwa kuzisoma na wazielewe ili wasiende nje ya kanuni za uendeshaji wa vikao vyao.

“Niiombe manejimenti hasa kuhusu suala la mapungufu ya matundu ya vyoo, ahakikishe anafanyia kazi yale tuliyokubaliana, tuchukue hatua kwa dhati kuhakikisha changamoto hii inapatiwa utatuzi wa haraka,”

“Zipo shule ukifika unaweza kusikitika kutokana na hali ilivyo mfano shule ya msingi Ndembezi ina matundu manne tu huku ikiwa na wanafunzi zaidi ya 1,000 na vyoo hivyo vinachangiwa kwa pamoja walimu na wanafunzi, hali hii siyo nzuri lazima hatua za kumaliza changamoto hii zianze mara moja,” ameeleza Mstahiki Meya.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Elias Masumbuko akizungumza na madiwani wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Getruda Gisema akizungumza kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani mjini Shinyanga.
Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga wakifuatilia kikao cha Baraza lao ambacho kimefanyika mjini Shinyanga.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Arnold Makombe (kushoto) na Katibu wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Ally Majeshi wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Shinyanga.