November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia: Wakati umefika wa nchi za Afrika kuondokana na migogoro

Na Penina Malundo, TimesMajira,Online

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema wakati umefika kwa nchi za Afrika kuondokana na migogoro na umaskini kutokana na rasilimali nyingi zilizopo huku zikijelekeza kujipindua kifikra, kimaarifa, kivitendo na kinadharia.

Amesema Itikadi ya kimapinduzi yenye lengo la kuwakomboa Wananchi wanyonge na kuziletea nchi maendeleo zilenge katika kuleta mageuzi na Mapinduzi ya kiuchumi ili iwe rahisi kuziunganisha na kuziwezesha kufikia dhamira hiyo.

Rais Samia ameyasema hayo leo Jumatano katika uzinduzi wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kibaha Mkoani Pwani .

Amesema kuwa Shule hiyo ya Uongozi ikitumika vyema itasaidia sana nchi husika kuandaa viongozi na makada ambao watandaliwa kiuongozi, kiitikadi, wakitanguliza uzalendo na Uafrika jambo ambalo litachochea harakati za kujiletea maendeleo, mabadiliko ya kifikra na mitazamo ambayo itakuwa ni chachu na chanya.

“Tunataka Vyama vyetu viwe na viongozi walioandaliwa vizuri, viongozi madhubuti wenye kufahamu nidhamu na miiko yao, ambao wataielewa, wataisimamia na kuielimisha jamii kuhusu itikadi yetu, Shule hii itusaidie kuzalisha akina Nyerere , Mandela, Samora Machel, Mzee Augustino Neto, Mzee Sam Nujoma, Mzee Mugabe na Mzee Kaunda huku tukienzi falsafa zao. Suala hili mimi naamini linawezekana na hasa kwa kuwa Vyama vyetu vina misingi ya kiitikadi inayofanana” Amesema Rais Samia

Aidha amesifu hatua ya uanzishwaji wa Shule hiyo ya uongozi ambayo itakuwa ni moja ya nguzo thabiti na ya kimkakati ya kudumisha ushirikiano wenye maslahi mapana katika kutoa mafunzo yenye uelewa wa pamoja kwa viongozi wa Vyama na Mataifa yao.

”Kupitia Shule hii ya Uongozi, viongozi na Makada wa Vyama na Mataifa haya na Watendaji wa Taasisi za kimkakati watapatiwa mafunzo ya muda mrefu, kati na mafupi ya uongozi ya aina zote ili kurithisha rika jipya la uongozi wa kimapinduzi Afrika.’’ amesema Samia

Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere Ujenzi wake umegharimu Dola za Marekani milioni 40 sawa na takriban Shilingi bilioni 100 za Tanzania. Fedha hizo ni ufadhili kutoka Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) kwa vyama sita vya Ukombozi Afrika ambavyo ni CCM (Tanzania) ,ANC (Afrika ya Kusini) , FRELIMO (Msumbiji), MPLA (Angola), SWAPO (Namibia) na ZANU-PF (Zimbambwe).

Shule ya Uongozi imepewa jina la Mwalimu Julius Nyerere, (Baba wa Taifa) ili kuenzi mchango wake ambae nyakati zote alikuwa ni miongoni mwa viongozi bora, imara, madhubuti, mtetezi wa wanyonge, Mwanamapinduzi na muumini mzuri wa itikadi na falsafa ya Uafrika (Pan-Africanism) aliyewahi kutokea katika Bara Afrika

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Vyama Rafiki, Serikali, Mabalozi wanaowakilisha nchi zao, watu mashuhuri wanachama, wapenzi, wakereketwa wa CCM na wananchi kwa ujumla.