November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waandishi wa habari wanawake washauriwa kuibua wawekezaji

Judith Ferdinand na Esther Macha, Timesmajira,Online Mbeya

WAANDISHI wa habari wanawake waliojikita kutangaza fursa za utalii na uwekezaji nchini wametakiwa kuandika habari za kuwaibua wawekezaji wadogo.

Aidha, jamii imeshauriwa kuthamini ilichonacho ili kuwekeza katika fursa mbalimbali kwa ajili ya kujiletea maendeleo binafsi na kwa taifa.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Shule ya Paradise Mission Pre and Primary, Ndele Mwaselela wakati akizungumza na waandishi wa habari wanawake kutoka vyombo mbalimbali nchini ambao wamefanya ziara ya kutangaza utalii na uwekezaji mkoani Mbeya.

Mwaselela,amesema wapo wawekezaji wengi nchini ambao ni wadogo, lakini hawafahamiki hivyo amewaomba waandishi hao kutumia kalamu zao kuwaibua ili waweze kuleta hamasa kwa jamii kujifunza na kuweza kuchukua hatua za kufanya uwekezaji kwa maendeleo yao binafsi na taifa kwa ujumla.

Amesema ili kufanikiwa katika uwekezaji wowote ule jamii hususani vijana wanapaswa kuzingatia mambo mbalimbali ikiwemo kuthaminin kile walichonacho hata kama ni kidogo.

Pia amewaraka kuwa na imani, ubunifu,uthubutu kuwa na kipaumbele cha mambo wanayotaka kufanya,kujenga mtandao kuwa tofauti kila siku pamoja na kupangilia ratiba.

Mkurugenzi wa shule ya Paradise Mission Pre and Primary,Ndele Mwaselela,akiwa katika picha ya pamoja waandishi wa habari wanawake kutoka vyombo na mikoa mbalimbali nchini, walipotembelea shule hiyo,ambao wapo katika ziara ya siku tatu mkoani humo kwa ajili ya kutangaza utalii na uwekezaji mkoani Mbeya.

Alisema ni muhimu kuzingatia matumizi mazuri ya fedha kuwa na uwezo wa kupangilia muda,ratiba,kujua biashara unayoenda kufanya umeifanyia utafiti wa kutosha kwa kufahamu changamoto zake, hasara na faida.

“Na ili kufanikiwa katika uwekezaji,lazima mradi unaoanzisha asilimia 95 uwe ni wa huduma za jamii ambazo ndizo zinazodumu na si rahisi kufa,”amesema Mwaselela..

Aidha amesema,uwezi kuchukua fedha kama ujajua mwelekeo wa maisha yako, hivyo wasichukue mkopo benki bila ya kujua biashara gani.

Sanjari na hayo alitumia fursa hiyo kuwapongeza waandishi wa habari wanawake kwa kuamua kutumia rasilimali zao kufanya ziara ya kutangaza utalii na fursa za uwekezaji nchini.

Alisema watu ambao wamekata taama na kushindwa kujua chanzo cha kupata fedha wanatumia kauli za kukatisha tamaa kuwa maisha ni haya haya na mengineyo.

“Kikubwa usikate tamaa,wala kusikiliza maneno ya kuwakatisha tamaa badala yake yachukueni na kiyatumia kama fursa ya kusonga mbele,”

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Raphael Group Limited, Raphael Ndelwa,amesema hakuna mafanikio rahisi lazima kuwekeza katika kujituma,hivyo amewaomba wadau kwenda kuwekeza katika Mkoa wa Mbeya kwani ni salama.

“Mbeya kuna usalama, mazingira mazuri pia kilimo,tunahitaji wawekezaji waje Mbeya, tujenge Mbeya na uchumi wetu,” amesema Raphael.

Mkurugenzi wa shule ya Paradise Mission Pre and Primary, Ndele Mwaselela,akizungumza na waandishi wa habari wanawake kutoka vyombo na mikoa mbalimbali nchini (hawapo pichani) waliotembelea shule hiyo,ambao wapo katika ziara ya siku tatu mkoani humo kwa ajili ya kutangaza utalii na uwekezaji mkoani Mbeya. picha na Judith Ferdinand.

Mratibu wa kampeni ya wanahabari wanawake kutoka mikoa mbalimbali ya kutangaza utalii na uwekezaji nchini, Mary Mwakibete,amesema lengo la kuanzisha kampeni hiyo ni kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kutangaza utalii pamoja na fursa za uwekezaji zilizopo katika mikoa mbalimbali nchini.

Amesema kampeni hiyo ilianza Agosti,2021 kwa kutembelea Mkoa wa Iringa hivyo kwa Mkoa wa Mbeya ni awamu ya pili na wataendelea hivyo kwa mikoa mingine.