Na Mwandishi wetu,Timesmajira,Online
KAMATI ya kupambana na kutokomeza ukatili Mkoa wa Dar es salaam kwa kushirikiana na shirika la kupambana na Ukatili la Jukwaa la Uti wa Mtoto (CDF) wameendesha kikao cha kujadili changamoto za ukatili wa kijinsia na watoto katika Mkoa huo.
Akizungumza jana na gazeti hili ,Ofisa Ustawi wa jamii Mkoa wa Dar es Salaam, Baraka Makona amesema licha ya Mkoa huo kushika nafasi ya nne kitaifa katika matukio ya ukatili, lengo lao kama Mkoa ni kutokomeza kabisa vitendo hivyo.
” Takwimu za ofisi ya Rais TAMISEMI zimebainisha kuwa katika kipindi cha miezi 9 iliyopita kulikuwa na takribani wahanga 3000 waliofanyiwa matukio ya ukatili katika Mkoa wa Dar es Salaam, kwahiyo tukaona kuwa licha ya kuwekwa nafasi ya nne kitaifa lakini hizi si takwimu nzuri kwa upande wetu na lengo letu ni kutokomeza kabisa vitendo hivi.” amesema Makona
Amesema lengo la kikao hiki ni kuwajulisha wajumbe kuhusu taarifa hiyo iliyotolewa na TAMISEMI pamoja na kuweka mikakati ya kupambana na ukatili katika ngazi zote kuanzia Halmashauri, Kata hadi ngazi za chini kabisa za mitaani ambapo vitendo hivi vimekuwa vikifanyika kwa kiasi kikubwa.
” Wananchi wanatakiwa kutambua kuwa vitendo hivi havifai kwani vinadhalilisha utu wa watoto na wanawake katika mkoa wetu kwaiyo kila mwananchi anatakiwa kushiriki kikamilifu kutoa taarifa kwa vyombo vya sheria pindi anapoona vitendo hivi vimefanyika ili kuhakikisha jamii yetu inakuwa salama muda wote,” amesema Makona
Naye Afisa ulinzi wa watoto kutoka shirika la CDF ,Sophia Temba amesema kuwa vitendo vya ukatili kwa mkoa wa Dar es Salaam vipo , hivyo dhumuni la kufanya kikao hiki ni kutoka na maadhimio ili kumfanya kila mtu kujua jukumu lake katika harakati za kupambana na ukatili kuanzia ngazi ya uongozi hadi wananchi.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote