Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online,Mwanza
VIONGOZI wa Kata ya Kayenze iliopo wilayani Ilemela mkoani Mwanza,wametakiwa kuhakikisha wanaimarisha suala la ulinzi na usalama wa eneo hilo.
Huku wananchi wa Kayenze wametakiwa kutoa ushirikiano kwa TANROADS katika suala zima la ujenzi wa barabara ili kuhakikisha barabara hizo zinakamilika kwa maendeleo ya wananchi wa Ilemela.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masala,wakati wa ziara yake yenye lengo la kujitambulisha ikiwa ni pamoja na kukagua miradi ya maendeleo.
Ambapo amekagua ukarabati wa ofisi ya idara ya uvuvi,ujenzi wa vyumba vya madarasa na vyoo katika shule ya msingi Kayenze pamoja na kuongea na wananchi wa Kata ya Kayenze katika mkutano wa hadhara kwa ajili ya kusikiliza kero na changamoto za wananchi na kuzipatia ufumbuzi.
Masala amesema viongozi wa Kata ya Kayenze wanapaswa kuhakikisha kuwa wanaimarisha suala zima la ulinzi na usalama.
Amesema maendeleo siku zote huja na maumivu na furaha, hivyo wananchi wa kata hiyo iwapo watahitajika kupisha barabara basi wahakikishe wanatoa ushirikiano.
Pia amesema,katika suala zima la kujikinga na Covid-19 amewahimiza wananchi kuchukua tahadhari kwa kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima,viongozi wa dini kuwatahadharisha waumini wao katika Nyumba za ibada huku walimu kuhakikisha wanawatahadharusha wanafunzi wao shuleni juu ya ugonjwa huo.
Masala alimuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kushughulikia suala la uhamisho wa walimu na kulipa kipaumbele huku akihakikisha kuwa anapata mrejesho juu pindi mfumo utakapofunguliwa.
Ili walimu waliohamishiwa katika shule za Kayenze wanahamia kwa haraka iwezekanavyo na kuweza kuondoa upungufu wa walimu katika kata hiyo na kata zingine.
Hata hivyo suala la upungufu wa madawati katika shule za Kayenze amemtaka Mtendaji wa kata hiyo kuhakikisha anashirikiana na wananchi ili kumaliza changamoto hiyo pamoja na kuweka wazi michango yote ya wananchi.
Aidha ametumia fursa hiyo kutoa maelekezo kwa OCD kuhakikisha kuwa fedha kiasi cha milioni 1.25, ambayo ilichangwa na wananchi wa Kayenze kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule zinarejeshwa kwa wananchi hao kwa ajili ya kuendeleza maendeleo katika kata yao.
Huku akimtaka mhusika kuziwasilisha fedha hizo katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya siku ya Ijumaa Julai 23 mwaka huu.
Kwa upande wake Ofisa Ardhi na Mipango Miji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Shukrani Kyando,amesema baadhi ya wananchi hawapo tayari katika kuchangia gharama za upimaji hivyo kusababisha zoezi la utoaji hati kusuasua kwani mchoro wa mipangomiji una viwanja 2400 na vimepimwa 800.
Huku waliolipia gharama za umilikishaji na kuandaliwa hatimiliki ni wananchi 27 tu,hivyo aliwahimiza na kuwahamasisha wananchi ambao hawajalipia gharama za upimaji na umilikishaji ili kulinda miliki zao kisheria.
Pia amewataka wananchi kufuata makubaliano yao na kamati za upimaji shirikishi huku akitolea mfano wa wananchi kuanza kujenga maeneo ambayo yaliachwa kwa ajili ya kupisha ujenzi wa barabara hivyo aliwataka kuacha kwani kinyume na hapo sheria namba 8 ya mwaka 2007 ya mipangomiji itatumika kuwaondoa.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Wilaya hiyo aliambatana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama, wataalam wa Halmashauri, wakuu wa taasisi mbalimbali, pamoja na viongozi wa Kata ya Kayenze.
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea