Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online, Dar
WATU zaidi ya watu 1,500 wamejitokeza na kupata huduma za bure za vipimo na matibabu katika hospitali ya KAM Musika kwa muda wa siku tatu ikiwa ni mpango wake wa kusaidia jamii.
Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi wa Hospitali ya KAM Musika, Dkt. Kandore Musika kwenye kambi maalum ya matibabu bure kwa wananchi mbalimbali.
Hospitali hiyo iliyoko Kimara Korogwe iliendesha kambi ya siku tatu ambapo zaidi ya watu 1,500 walichunguzwa afya zao na kupatiwa matibabu bila malipo.
Dkt. Musika amesema kwa kuwa hospitali hiyo ni mpya imejielekeza kutoa huduma zaidi kwa wananchi badala ya kuangalia biashara kwani Watanzania wengi hawawezi kumudu gharama za vipimo na matibabu.
Amesema kila mwaka Hospitali ya KAM Musika itakuwa ikitenga wiki maalum kwa Watanzania kwenda kufanyiwa vipimo na kupatiwa matibabu bure kama sehemu ya mchango wake kwa jamii.
Amesema kwenye kambi hiyo wamepima na kuwabaini watu mbalimbali wenye magonjwa kama UTI, malaria, kuhara, sukari, shinikoizo la damu na maradhi mbalimbali ya macho.
“Ni vizuri sana kupima mara kwa mara kujua afya yako ili uweze kutibiwa kabla hali haijawa mbaya sana kwa mfano kwenye hii kambi tumegundua watu wengi wenye sukari na shinikizo la damu ambao walikuwa hawajui sasa hii ni mbaya sana kwa afya,” ameshauri Dkt. Musika
Amrsema KAM hospital itajitahidi kuwasaidia Watanzania kwa kuhakikisha inawahudumia kwa gharama nafuu za vipimo na matibabu ili wengi wajitokeze kupima afya zao na kutibiwa.
Amesema ili kuepukana na maradhi mbalimbali pia wananchi wanashauriwa kula chakula chenye mlo kamili wenye protini, vitamin na wanga ili kuhakikisha wanakuwa na afya bora.
Amesema wanapaswa pia kusafisha mazingira ya kuishi kuhakikisha hakuna maji yanayotuamana ambayo hutengeneza mazalia ya mbu na kusababisha maradhi yaa kuhara na kichocho.
Mmoja wa wanufaika wa matibabu hayo, Ndumaeli Ulomi aliishukuru hospitali ya KAM kwa kutoa vipimo na matibabu ya bure akisema kuwa si watanzania wote wanamudu huduma hizo.
“Tunaomba wengine nao waige mfano huu kwasababu watanzania wengi wanashida ila hawana uwezo wa kugharamia vipimo na matibabu tunawashukuru sana na waendelee na moyo huu wa kuwasaidia watanzania,” amesema
Scarion Marcel ambaye naye alinufaika na huduma hizo za bure, aliishukuru Hospitali ya KAM kwa kutenga wiki ya huduma bure za vipimo na matibabu kwani watanzania wengi wasio na uwezo wamenufaika na huduma hizo.
“Kwa kweli hii inastaajabisha kuona hospitali inajitolea kuchunguza wagonjwa na kuwatibu bure iwapo watanzania wengi watakuwa na moyo kama huu nchi itafika pazuri kwasababu watu wengi wasio na uwezo watanufaika,” amesema
More Stories
Watakiwa kushirikiana kutikomeza matatizo ya lishe
CCBRT yazidi kuunga mkono juhudi za Rais Samia
Madaktari bingwa wa Samia watua Rukwa