Judith Ferdinand, TimesMajira Online,Mwanza
TAKRIBANI wagonjwa 900 hadi 1,200, wakiwemo watoto na watu wazima, unufaika na huduma za matibabu ya moyo kwa mwezi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando.
Hayo yameelezwa leo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando Dkt.Samson Kichiba,wakati hospitali hiyo ikiungana na Dunia kuadhimisha Siku ya Moyo Duniani ambayo ufanyika kila ifikapo Septemba 29 ya kila mwaka,ambapo amewahimiza wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara ili kuepuka madhara yatokanayo na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ukiwemo ugonjwa wa moyo.

Dkt.Kichiba amesema,wagonjwa hao wasipopata matibabu kwa wakati wanaweza kupata kiharusi au moyo kushindwa kufanya kazi huku akisitiza kuwa kaulimbiu ya mwaka huu ni “Kila pigo la moyo ni maisha, lilinde usilipoteze,” inalenga kutuhamasisha kuilinda mioyo yetu kwa kuzingatia miongozo ambayo wataalamu wanaelekeza ili kuwa na afya njema kama vile kufanya mazoezi, kuzingatia lishe bora na kuchunguza afya zetu mara kwa mara ili kujua namba zetu,”
Amesema,ili kuimarisha huduma za moyo Serikali kupitia Wizara ya Afya inahakikisha taasisi za utafiti, vyuo vikuu, vituo vya huduma na watafiti wengine zitaendelea kufanya tafiti katika magonjwa ya moyo hapa nchini zitakazotusaidia kufanya maamuzi ya kisera yenye uthibitisho wa kisayansi unaoendana na mahitaji ya nchi yetu.
Aidha amewaomba wadau kuendelea kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya magonjwa ya moyo, huku Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando ikiahidi kuendelea kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa upasuaji wa kifua na moyo Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando,Dkt.Shija Mahenda amesema,katika hospitali hiyo upande wa kliniki ya moyo ya watoto pekee hupokea watoto kati ya 200 hadi 250 kwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo kila mwezi.
“Kati ya watoto hao zaidi ya asilimia 40 huwa na changamoto za magonjwa ya moyo.Huku asilimia 75 ya magonjwa ya moyo kwa watoto ni ya kuzaliwa na wengi wao huja wakiwa wamechelewa kufika hospitalini kwa wakati,”amesema Dkt.Mahenda.
Amesema,uchunguzi wa mapema unaweza kusaidia kubaini changamoto za kiafya na kuwawezesha wahudumu wa afya kutoa ushauri, uchunguzi zaidi na matibabu kwa wakati huku akihimiza ulaji wa lishe bora, kufanya shughuli za mwili,kuepuka matumizi ya tumbaku, vileo na kupunguza vihatarishi vingine vya magonjwa
Naye Neema Mwita, mmoja wa wananchi waliojitokeza kupima afya katika maadhimisho hayo amesema, vipimo vimemsaidia kujua hali yake ya kiafya huku akiwahimiza wananchi kuwa na utaratibu wa kupima afya mara kwa mara ili kujua hali zao na kuchukua hatua mapema.
Mwita amesema,baadhi ya wananchi huogopa kupima kwa kuhofia kugundulika kuwa wana magonjwa, hivyo akashauri wapewe elimu kuhusu umuhimu wa kupima afya.
Hata hivyo Mary Clement amesema,gharama za vipimo ni changamoto kwa baadhi ya wananchi, lakini kupitia maadhimisho hayo ameweza kupata huduma hiyo. Aliwahimiza wananchi kupima afya ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na kutokujua hali zao.



More Stories
Maonesho Tech, AI yatakiwa kuleta matokeo, Yas yajizatiti
Serikali yasisitiza utekelezaji mpango ualbino
Wafugaji wasiosajiliwa Kibiti watakiwa kuondoka