September 29, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yasisitiza utekelezaji mpango ualbino

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Dar

SERIKALI imewataka wadau kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Ustawi wa Watu Wenye Ualbino (MTHUWWU), ili kuhakikisha unatekelezwa kwa vitendo, kwa wakati na kwa kuzingatia afua zilizowekwa.

Wito huo umetolewa jijini Dar-es-Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi, wakati akifungua Jukwaa la Kitaifa la Uratibu na Utekelezaji wa MTHUWWU.

Amesema,Serikali na wadau wanapaswa kuhakikisha mpango huo haubaki kwenye nyaraka, bali unatekelezwa kwa vitendo, ukipewa rasilimali zinazohitajika na shughuli zilizopangwa kutekelezwa kwa wakati.

“Ni kuweka mipango madhubuti muhimu ya utekelezaji wa mpango na kusaidia afua zilizoainishwa katika mpango zinapatiwa utekelezaji na kutekeleza kwa wakati,”amesema Prof.Kabudi.

Amesema,shughuli zilizopangwa zinapaswa kutekelezwa na taarifa zake kutolewa kwa wakati ili kuiwezesha Serikali na wadau kubaini changamoto, kupima matokeo na kuchukua hatua za kuboresha utekelezaji.

Prof.Kabudi amesema,mpango huo una nguzo nne ambazo ni ulinzi, kinga, usawa na kutobagua pamoja na uwajibikaji, huku mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ukitakiwa kufanya kazi kuanzia ngazi ya Taifa hadi Mkoa, Halmashauri, Kata, Kijiji na Mtaa.

Awali, Ofisa Ustawi wa Jamii Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Joy Maongezi amesema,Serikali imetenga kiasi cha sh.milioni 90 kwa ajili ya ununuzi wa mafuta kinga dhidi ya ugonjwa wa ngozi kwa watu wenye ualbino, akisisitiza kuwa hatua hiyo inapaswa kwenda sambamba na utekelezaji wa mipango yote inayolenga kuboresha ustawi wa watu wenye ualbino.

“Fedha hizi zimetengwa katika mwaka wa fedha 2025/26 kwa ajili ya ununuzi wa mafuta hayo kupitia Bohari ya Dawa (MSD), ambapo tayari chupa 339 zimesambazwa katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro,”amesema.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Watu Wenye Ulemavu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wambura Kizito amesema,sasa ni wakati wa kutoka katika hatua ya kuwa na mpango kazi na kuingia kwenye utekelezaji unaopimika, unaoratibiwa na wenye wajibu.

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Kitaifa la Uratibu na Utekelezaji wa MTHUWWU, Yohana Sali amesema,jukwaa hilo litawasilisha kwa Serikali na wadau changamoto, fursa na vipaumbele vya utekelezaji wa mpango huo, huku akibainisha kuwa kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Tanzania Bara ina watu wenye ualbino 71,631, wakiwemo wanaume 41,203 na wanawake 30,428.