October 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wajumbe Mamlaka waridhishwa ujenzi wa shule mpya Mlowo.

Na Moses Ng’wat, Mlowo

WAJUMBE wa Baraza la Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mlowo, wilaya ya Mbozi, mkoa wa Songwe, wameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari katika kitongoji cha Lutumbi Kiwandani, ambao umefikia asilimia 65.

Wajumbe hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa mamlaka hiyo, Bosco Njate, wametembelea mradi huo leo, Oktoba 23, 2026, na kujionea hatua iliyofikiwa, huku ujenzi ukitarajiwa kukamilika Novemba 26, mwaka huu.

Ziara hiyo imefanyika muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao cha baraza kilichofanyika katika Shule ya Sekondari Dkt. Samia Mlowo.

Akizungumza kwa niaba ya wajumbe, Diwani wa Kata ya Mlowo, Jackson Mwanda, ametoa wito kwa wadau kuendelea kuunga mkono mradi huo ili ukamilike kwa wakati na kuanza kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwakani.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa mamlaka hiyo, Peter Nkeka, ambaye pia ni Mtendaji wa Kata ya Mlowo, amesema ujenzi huo ni muhimu kutokana na ongezeko la mahitaji ya miundombinu ya elimu katika kata hiyo yenye wakazi 66,446 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Amesema ujenzi wa shule hiyo unagharimu Sh milioni 583, fedha zilizotolewa na Serikali Kuu kupitia programu ya BOOST.

Msimamizi wa mradi huo, Mwalimu Renatus Mwakitalu, amesema ujenzi ulianza Agosti 8, mwaka huu, na hadi sasa umefikia asilimia 65, huku ukitarajiwa kukamilika Novemba 26.

Amesema shule hiyo, ambayo bado haijapewa jina, itakuwa na uwezo wa kupokea wanafunzi 400 na inatarajiwa kuanza kutoa huduma mwaka 2027.