November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TBS yawapongeza wachezaji wake, wajipanga kutwaa mataji

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

WACHEZAJI wa timu ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) walioshiriki Mashindano ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma na Makampuni binafsi Tanzania (SHIMMUTA) mkoani Tanga wamepongezwa kwa jinsi walivyoshiriki na kutoa ushindani mkali katika michuano hiyo na kufanikiwa kutwaa baadhi ya mataji.

Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi wa Upimaji na Ugezi, Mhandisi Johanes Maganga wakati alipokuwa akizungumza na wachezaji wa shirika hilo walioshiriki mashindano ya SHIMMUTA yaliyomalizika mwishoni mwa wiki.

Amesema, ameridhishwa na jinsi wachezaji walivyojituma kwenye mashindano hayo yaliyokuwa na ushindani mkubwa na kufanukiwa kushinda baadhi ya mataji huku pia akiwataka wachezaji wa timu za Shirika hilo kuendelea kufanya mazoezi na kupata timu bora ambazo zitaweza kutwaa mataji katika mashindano yajayo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Yusuf Ngenya amesema kuwa, shirika hilo limeshirika mashindano hayo kwa miaka sita mfululizo na kuna mengi wamejifunza si kwa upande wa michezo pekee bali pia hata kubadilishana uzoefu katika kazi na kujenga mahusiano bora.

“Kwanza michezo inaleta afya na inasaidia kuleta ufanisi kwani katika kazi zao za kila siku zinakwenda vizuri kutokana na utendaji wa pamoja jambo linaloongeza ufanisi katika kazi, ” amesema Dkt. Ngenya.

Katika mashindano hayo wachezaji wa timu ya TBS walitwaa baadhi ya mataji, ambapo kwenye mashindano ya kuvuta kamba timu ya wanaume iliweza kushika nafasi ya tatu huku katika mpira wa pete wanaume, katika kundi lake TBS alikuwa na timu nne kutoka SUA, DUCE, TANESCO na katika michezo yake, TBS iliifunga SUA seti 2-0, DUCE seti 2-0 na kuingia robo fainali.

Licha ya kutinga hatua hiyo lakini walishindwa kusonga mbali baada ya kufungwa na timu ya Mamlaka ya Wanyama Pori Ngorongoro. Katika mchezo wa drafti kwa wanawake timu hiyo iliibuka mshindi wa tatu baada kupata ushindi dhidi ya Muhimbili.

Kwa upande wa mpira wa pete kwa wanawake, TBS walikuwa kundi moja Mbeya-AUWASA, TMDA, SUA, NHIF na TANESCO na katika mchezo yake TBS iliibuka na ushindi wa goli 23-21 dhidi ya Mbeya AUWASA, waliwafunga TMDA goli 50-2 kisha, waliwafunga SUA goli 36-22 na kutonga robo fainali ambapo kwenye mchezo wa robo fainali timu hiyo ilifungwa na UDOM na kutolewa nje ya mashindano.

Kwenye soka wanaume, TBS alikuwa pamoja na timu za TBS, DUCE, KCMC, TRA na DIT ambapo waliwafunga DUCE goli 4-0, wakatoka sare 0-0 na KCMC, lakini timu hiyo ilitolewa hatua za makundi baada ya mashindano hayo na TBS ilitwaa mataji mawili.