October 28, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Camfed yawashika mkono wasichana waliokatisha masomo Handeni

Na Mwandishi Wetu

WATOTO wa kike waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali katika Wilaya ya Handeni mkoani Tanga wamepata matumaini mapya baada ya kurejea shuleni kwa msaada wa Shirika la CAMFED, hatua inayowapa fursa ya kuendelea na elimu na kutimiza ndoto zao.

Elimu imeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kubadili maisha ya watoto na vijana, kwa kuwa huwapa maarifa, ujuzi na fursa ya kujenga maisha yenye mwelekeo mzuri.

Kwa baadhi ya wasichana waliorejea shuleni, safari hiyo haikuwa rahisi. Wengine walikatisha masomo kutokana na changamoto za kifamilia, mahitaji ya shule, ujauzito na mazingira ya kijamii, lakini baada ya kupata nafasi ya kurejea wameanza kujenga upya ndoto zao.

Nimerudi kwa nguvu kubwa

Lucy Adam (sio jina lake halisi), mwanafunzi wa Kidato cha Pili katika Shule ya Sekondari Kwamatuku, Wilaya ya Handeni, ni miongoni mwa wasichana waliokatisha masomo na baadaye kurejea shuleni.

Anasema kipindi alichokuwa nyumbani kilikuwa kigumu, lakini kurejea shuleni kumempa nguvu mpya ya kusoma na kuboresha mwenendo wake wa kitaaluma.

“Kipindi nilipokuwa nyumbani maisha yalikuwa magumu, lakini nimerudi shule najiona mtu mwenye mabadiliko. Hivyo hapa nilipo nasoma kwa kujituma kuliko ilivyokuwa mwanzo,” anasema.

Lucy anasema ndoto yake ni kuwa mwanajeshi, kazi ambayo amekuwa akiipenda tangu akiwa mtoto.

“Ni ndoto ambayo natamani kuifikia kama binti mwenye matamanio ya elimu yake. Ndiyo sababu nilipokatisha masomo yangu niliumia, kwani nyumbani nilikaa kwa muda wa mwaka mmoja. Lakini sasa nimerejea kwa nguvu kubwa ya kusoma kwa bidii,” anasema.

Ujauzito haukumzuia Adelina kurejea shule

Adelina Joseph (sio jina lake halisi), mwanafunzi wa kidato cha nne Shule ya Sekondari Kwamatuku, naye ni miongoni mwa wasichana walionufaika na fursa ya kurejea shuleni.

Anasema awali alikuwa akifanya vizuri katika masomo, lakini changamoto za kifamilia na ukosefu wa mahitaji muhimu ya shule vilimfanya aingie katika mahusiano, hali iliyosababisha kupata ujauzito na hatimaye kuacha shule.

Baada ya kujifungua, Adelina bado alikuwa na kiu ya kuendelea na masomo, lakini uwezo wa familia yake haukuruhusu.Anasema baba yake alifanya mawasiliano na CAMFED na ndipo alipata fursa ya kurejea shuleni.

“Baba alianza kufanya mawasiliano na Shirika la CAMFED kuwa linasaidia watoto wa kike ndipo niliporudi shule na kuanza masomo, kwa sababu ndoto yangu ilikuwa kusoma mpaka sasa naendelea kujituma zaidi ili kufikia malengo yangu,” anasema.

Adelina anasema kurejea shuleni kumemrudishia furaha na matumaini, kwani elimu ilikuwa moja ya malengo makubwa aliyokuwa amejiwekea.

Anasema kupitia ufadhili huo anapata mahitaji mbalimbali, ikiwemo ada, chakula, madaftari, sare na vifaa vingine muhimu vya shule.

“Ninaishi hapa hapa shuleni, ufadhili ninaopata CAMFED ni pamoja na kulipiwa ada, chakula, daftari, nguo za shule na vifaa vingine muhimu. Toka nimerudi baada ya kukatisha masomo, najiona nina mabadiliko makubwa.

Nipo tofauti na maisha ya nyuma na ndio sababu ninajituma sana kusoma ili niwe mfano kwa wengine, lakini hapa shule ninaishi kwa amani kubwa inayonifanya nifurahie masomo yangu “anasema.

Adelina anasema ndoto yake ni kusoma na kuwa daktari ili kuwasaidia watu wenye changamoto mbalimbali za kiafya.

Walimu wazungumzia mabadiliko

Mwalimu wa Shule ya Sekondari Kwamatuku iliyopo kata ya Kwamatuku anayesimamia Kitengo cha Mradi wa Elimu ya Watu Wazima (SEQUIP AEP) Wilaya ya Handeni, Prisca Daudi, anasema jukumu lake ni kuhakikisha wasichana waliorejea shuleni wanapata mahitaji muhimu na msaada wa kitaaluma na kisaikolojia.

Anasema baadhi ya wasichana hao wanatoka katika familia zenye changamoto, hivyo wamekuwa wakipewa ushauri na kufuatiliwa ili kuhakikisha wanatumia ipasavyo mahitaji wanayopatiwa.

“Kupitia kitengo changu mimi ni mlezi na mshauri katika masuala ya kitaaluma. Katika wasichana wangu hawa, kuna wengine wana changamoto za kifamilia walikotoka, hivyo nimekuwa nikiwapa ushauri na kuwafuatilia kujua mahitaji yao kama wameyapata na wanayatumia vipi,” anasema.

Kwa upande wa taaluma, Prisca anasema shule imekuwa ikihakikisha wasichana hao wanahudhuria vipindi kama wanafunzi wengine, huku mahudhurio yao yakifuatiliwa.

Anasema pia hakuna unyanyapaa dhidi ya wanafunzi waliorejea shuleni, huku baadhi yao wakifanya vizuri na kuwa mfano kwa wenzao.

“Hawa wasichana wamekuwa mfano wa kuigwa. Wakiona wenzao wanaelekea kupata changamoto fulani, wanatoa taarifa mapema kwa walimu. Hivyo wamekuwa chachu ya mabadiliko kwa wenzao kutokana na stadi za maisha walizopitia,” anasema.

Prisca anasema CAMFED imekuwa ikiwasaidia wasichana wanaotoka katika mazingira magumu kwa kuwapatia mahitaji muhimu ya shule na kuwawezesha kuishi katika mazingira yanayowawezesha kuzingatia masomo.

Wito kwa wasichana

Mwalimu mlezi wa CAMFED katika Shule ya Sekondari Kwamatuku, Dativa Patrick, anasema wamekuwa wakifanya vikao na wasichana hao ili kutambua changamoto zao na kupunguza utoro.

Anawataka wanafunzi wanaofadhiliwa na CAMFED kuthamini fursa hiyo na kujituma katika masomo ili waweze kujikomboa kielimu na kiuchumi.

Hata hivyo, anasema bado kuna haja ya kuongeza idadi ya wasichana wanaonufaika na ufadhili huo.

“Ombi letu kwa CAMFED ni kupata ufadhili zaidi kwa wasichana ili wengi waweze kusoma, kwa kuishi bweni au kupanga vyumba,” anasema.

Dativa anasema baadhi ya changamoto zinazowakabili wasichana ni ujauzito na kufeli mitihani kidato cha pili, lakini baada ya kupata fursa ya kurejea shuleni wameonyesha utayari wa kuendelea na masomo kwa ari kubwa.

Mafanikio kielimu kwa wanafunzi

Katika shule hiyo, mmoja wa wanafunzi wanaofadhiliwa na CAMFED ambaye yupo kidato cha nne amekuwa kinara wa kufanya vizuri kwa kuongoza kufanya vizuri kwa kidato cha nne chote kutokana na kuonyesha utayari wa kusoma kwa bidii.

CAMFED na Halmashauri zaendelea kushirikiana

Mratibu wa CAMFED na Afisa Elimu, Vifaa na Takwimu wa Idara ya Elimu Sekondari Wilaya ya Handeni, Noel Kombo, anasema kuna utaratibu wa serikali unaowapa fursa wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali kurejea shuleni.

Anasema CAMFED imekuwa ikishirikiana na Halmashauri kuhakikisha wasichana wenye utayari wa kurejea shuleni wanapata msaada unaowawezesha kuendelea na elimu.

Kwa mujibu wa Kombo, Shule ya Sekondari Kwamatuku ina wanafunzi wanane waliorejea katika mfumo huo, ambapo watatu kati yao wanafadhiliwa na CAMFED.

Anasema Halmashauri imekuwa ikikusanya takwimu na kufanya ufuatiliaji wa wanafunzi waliorejea shuleni, huku ikitoa elimu kwa jamii kuhusu fursa zilizopo kwa watoto waliokatisha masomo.

“Sisi kama wasimamizi wa elimu tunaendelea kuhamasisha hilo ili lengo la Serikali liweze kutimia na wanafunzi waliokatisha ndoto zao waweze kurudi shule na kutimiza kile ambacho walikuwa na kiu nacho,” anasema.

Kombo anasema jumla ya shule 25 za sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni zinapata ufadhili kutoka CAMFED.

Anaitaja Shule ya Sekondari Gwekizinga kuwa miongoni mwa shule hizo, ambapo tangu mwaka 2024 wanafunzi sita waliokatisha masomo wamepata fursa ya kurejea shuleni na, kwa mujibu wake, wameendelea kufanya vizuri.

Fursa ya kurejea shuleni imekuwa hatua muhimu kwa wasichana waliokatisha masomo kutokana na changamoto mbalimbali kwao, kurejea darasani si mwanzo mpya wa elimu pekee, bali pia ni nafasi ya kurejesha matumaini na kuendelea na safari ya kutimiza ndoto zao.

CAMFED ni shirika la kimataifa lisilo la kiserikali (NGO) linalojulikana kama Kampeni ya Elimu ya Kike (Campaign for Female Education), ambalo lilianzishwa mwaka 1993 lenye lengo la kutokomeza umaskini na ukosefu wa usawa kupitia elimu ya wasichana na uwezeshaji wa wanawake vijana barani Afrika.

Shughuli na Malengo Makuu ya CAMFED
Nchini Tanzania, shirika hili limekuwa likifanya kazi kwa karibu na serikali kupitia Wizara ya Elimu na TAMISEMI kusaidia maelfu ya wanafunzi katika shule za serikali kwenye mikoa mbalimbali.