Na Joyce Kasiki, Dodoma



WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi, amewataka watumishi wa umma wanaofanya kazi katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma kutumia majengo na miundombinu ya kisasa iliyowekwa kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa wananchi, badala ya kujikita katika kufurahia uzuri wa majengo hayo.
Prof. Kabudi amesema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa majengo ya wizara na taasisi za Serikali pamoja na barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Amesisitiza kuwa uwekezaji huo unapaswa kuonekana kupitia matokeo chanya katika utendaji wa Serikali na ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Amesema majengo mazuri pekee hayatoshi kuleta mabadiliko yanayotarajiwa bila kuwapo kwa uwajibikaji, uadilifu, ubunifu, nidhamu ya kazi na uzalendo miongoni mwa watumishi wa umma.
Kwa mujibu wa Prof. Kabudi, mazingira bora ya kufanyia kazi yaliyowekwa na Serikali yanapaswa kuwa chachu ya kuongeza ufanisi, kurahisisha utekelezaji wa majukumu na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zaidi.
“Majengo mazuri pekee hayatoshi, tunahitaji pia utendaji bora, nidhamu ya kazi na uzalendo ili wananchi waone matokeo ya uwekezaji huu kupitia huduma bora za Serikali,” amesema.
Amesema uwepo wa wizara na taasisi za Serikali katika eneo moja utarahisisha uratibu wa shughuli za Serikali, mawasiliano na ushirikiano baina ya taasisi, pamoja na kupunguza changamoto zinazotokana na kutawanyika kwa ofisi katika maeneo mbalimbali.
Ameongeza kuwa barabara za lami katika mji huo zitaimarisha usafiri, mawasiliano na upatikanaji wa huduma, huku zikiunganisha maeneo mbalimbali ndani na nje ya Mji wa Serikali.
Kwa mujibu wa Prof. Kabudi, maendeleo ya Mji wa Serikali Mtumba pia yanafungua fursa za kiuchumi kwa sekta binafsi na wananchi kupitia ongezeko la mahitaji ya huduma za usafirishaji, malazi, biashara na huduma za kitaalamu.
Amewahimiza wawekezaji na wafanyabiashara kutumia fursa hizo kuwekeza katika Mji wa Serikali na Dodoma kwa ujumla, akieleza kuwa ukuaji wa shughuli za Serikali unaweza kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Amesema ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya Mtumba ni sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha hadhi ya Dodoma kama Makao Makuu ya nchi na kuweka mazingira yatakayowezesha Serikali kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Katika taarifa hiyo, wananchi, hususan wakazi wa Mkoa wa Dodoma, wamehimizwa kujitokeza kushuhudia uzinduzi wa majengo ya wizara na taasisi za Serikali pamoja na barabara za lami. Tukio la upigaji fataki limepangwa kufanyika usiku wa Oktoba 30, 2026, kuelekea uzinduzi huo.

More Stories
Viongozi TNCM wapewa mafunzo ulinzi wa wananchi
iTrust yazindua mifuko mitatu ya Uwekezaji
TTB yazindua kampeni ya Utalii wa Ndani