October 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenge wataka daraja Ileje kukamilika kwa wakati

Na Moses Ng’wat, Ileje

KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, amewataka wakandarasi wanaojenga daraja la Mto Isenga wilayani Ileje kuongeza kasi ya ujenzi ili likamilike kwa wakati, akionya kuhusu uwezekano wa mvua kubwa za El Nino.

Mwang’onda ametoa wito huo, Oktoba 7, 2026, baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wake na kuweka jiwe la msingi katika mradi huo unaounganisha Kijiji cha Ilanga, Kata ya Mlale wilayani Ileje na Kijiji cha Namwangwa wilayani Mbozi.

Amesema mradi huo wenye thamani ya Sh bilioni 2.8 unapaswa kutekelezwa kwa kuzingatia muda, ubora na thamani ya fedha, ili wananchi waanze kunufaika na kwa wakati.

“Ni muhimu mradi huu ukamilike kwa wakati na kwa kuzingatia ubora unaotakiwa, kwa sababu wananchi wanautegemea katika shughuli zao za kila siku,” amesema Mwang’onda.

Aidha, amewataka wakandarasi na wasimamizi wa mradi huo kutumia vifaa vinavyokidhi viwango pamoja na wataalamu wenye sifa, akisisitiza kuwa fedha za Serikali zilizotengwa kwa mradi huo zinapaswa kuleta matokeo yenye manufaa ya muda mrefu.

Mwang’onda amesema maandalizi ya kukabiliana na mvua kubwa na mafuriko yanapaswa kufanyika mapema, akieleza kuwa hali hiyo inaweza kuathiri kasi ya ujenzi na kusababisha uharibifu wa miundombinu iwapo tahadhari hazitachukuliwa.

Amesema utekelezaji wa mradi huo kwa wakati utasaidia kuimarisha mawasiliano kati ya wananchi wa Ileje na Mbozi, huku ukirahisisha usafirishaji wa mazao na bidhaa.

Kukamilika kwa daraja hilo pia kunatarajiwa kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo yanayounganishwa na mradi huo.