Na Zena Mohamed,TimesMajira Online,Dodoma
SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linaendelea na utekelezaji wa miradi ya kufikisha gesi asilia katika maeneo yenye viwanda, ikiwemo Mradi wa Bomba la Gesi Asilia kutoka Kinyerezi jijini Dar es Salaam hadi Chalinze mkoani Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo Septemba 21, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame,amesema mradi huo unalenga kufikisha gesi asilia kwa njia ya bomba hadi Chalinze ili kuhudumia Kongani za Viwanda za Mkoa wa Pwani.
Amesema maeneo yatakayofikiwa na mradi huo ni pamoja na Kongani za Viwanda za Zegereni na Kwala, pamoja na viwanda vingine vinavyoendelea kujengwa katika maeneo hayo.

Makame amesema mkuza wa ujenzi wa mradi huo tayari umepatikana, huku kazi zinazoendelea kwa sasa chini ya Mshauri elekezi zikiwa ni Upembuzi Yakinifu wa mradi ambao umefikia asilimia 90.4.
Aidha,amesema kuwa tatmini ya athari kwa Mazingira na Jamii imefikia asilimia 81, na baada ya kukamilika kwa kazi hizo, taratibu za kumpata Mkandarasi wa ujenzi zitaendelea.
Hata hivyo Makame amesema TPDC imeanza pia majadiliano na wawekezaji kuhusu teknolojia ya miradi midogo ya kubadili gesi asilia kuwa kimiminika (Mini-LNG), inayowezesha gesi kusafirishwa kwa malori maalum kwenda maeneo yasiyo na miundombinu ya mabomba.

Ambapo amesema hadi sasa mazungumzo yanaendelea na kampuni sita, ambapo TPDC tayari imesaini makubaliano ya mauziano ya gesi asilia na kampuni tatu, ambazo zinaendelea na hatua mbalimbali za utekelezaji, ikiwemo kukamilisha ununuzi wa ardhi na Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii kabla ya kutafuta Wakandarasi wa ujenzi.
“Teknolojia hii imethibitika kibiashara kuwa na uwezo wa kufikisha gesi asilia zaidi ya kilomita 500 kwa faida, hatua inayolenga kuwezesha gesi asilia kufikishwa katika maeneo mbalimbali nchini.

More Stories
TANESCO yafafanua mikakati kukabiliana na El Niño
Kingoba :Hakuna Habari yenye thamani kuliko maisha ya Mwandishi
TANESCO yatakiwa kuongeza ubunifu katika utafiti na mipango