September 21, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANESCO yafafanua mikakati kukabiliana na El Niño

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limeeleza mikakati mbalimbali inayoendelea kutekelezwa kukabiliana na athari za mvua za El Nino zinazotarajiwa kuanza hivi karibuni, ikiwemo kuimarisha miundombinu ya umeme pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi salama ya umeme wakati wa mvua.

TANESCO imeeleza kuwa hatua hizo zinalenga kuhakikisha huduma ya umeme inaendelea kupatikana kwa usalama na kwa uhakika, huku wananchi wakichukua tahadhari dhidi ya hatari inayoweza kujitokeza katika kipindi cha mvua.

Hayo yameelezwa katika mahojiano maalumu na wataalamu mbalimbali wa TANESCO yaliyofanyika katika vipindi mbalimbali vya Radio na Televisheni, kwa lengo la kuelimisha umma kuhusu maandalizi na mikakati ya TANESCO katika kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo.

Akizungumza katika kipindi cha 360 kinachorushwa na moja ya Televisheni nchini, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO,Irene Gowelle, amesema Shirika linaendelea na hatua mbalimbali za kuimarisha miundombinu ya umeme ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua za El Nino.

“Kwa sasa TANESCO inaendelea na ukaguzi na uimarishaji wa miundombinu ya umeme katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo kubadilisha nguzo zilizoharibika na kuweka nguzo imara, kukagua hali ya nyaya za umeme, pamoja na kukata miti inayokaribia au kugusa njia za umeme,” amesema Gowelle.

Ameongeza kuwa TANESCO pia inaendelea kukagua vituo vya kupokea na kupoza umeme pamoja na mazingira yanayozunguka miundombinu hiyo, hatua inayolenga kuhakikisha mfumo wa upatikanaji wa umeme unaendelea kuwa salama katika kipindi cha mvua.

Kwa upande wake, Meneja wa Afya na Usalama Kazini , Mhandisi Fred Kayega, amesema maji na vitu vyenye asili ya chuma vinaweza kurahisisha upitishaji wa umeme, hivyo wananchi wanapaswa kuwa makini zaidi wakati wa mvua na mafuriko.

“Tunasisitiza wananchi kutogusa nyaya za umeme zilizoanguka chini, hasa wakati wa mvua au mafuriko. Wananchi wanapaswa kujiweka mbali na eneo hilo na kutoa taarifa TANESCO ili wataalamu wafike na kuchukua hatua za haraka ,” amesema Mhandisi Kayega.

TANESCO inaendelea kuwahimiza wananchi kushirikiana na Shirika kwa kutoa taarifa mapema wanapoona miundombinu ya umeme iliyo katika hali isiyo salama, ikiwemo nguzo, nyaya zinazoning’inia au kuanguka chini, pamoja na miti inayoonekana kugusa Nyaya au nguzo za umeme ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.