Na Zena Mohamed,TimesMajira Online, Dodoma
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) inalenga kuzalisha takribani wahitimu 5,635,529 ifikapo mwaka 2050, watakaokuwa na ujuzi unaohitajika katika sekta mbalimbali za uchumi, ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Hayo yameelezwa jijini hapa leo,Septemba 4,2026 na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo katika mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27.

Kasore amesema VETA ina nafasi kubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga Tanzania yenye uchumi imara, jumuishi na shindani, watu wenye uwezo, matumizi ya teknolojia pamoja na mazingira yanayolindwa kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Amesema katika kutekeleza Nguzo ya kwanza ya Dira hiyo inayohusu uchumi imara, jumuishi na shindani, VETA inalenga kuhakikisha inazalisha nguvu kazi yenye ujuzi itakayoweza kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Kwa mujibu wa Kasore, mafunzo hayo yataelekezwa zaidi katika sekta za kimkakati zikiwemo uchumi wa buluu, uzalishaji, ujenzi na miliki, nishati, madini, uchakataji wa mazao ya kilimo, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), lojistiki na huduma za kibiashara.

Aidha, amesema VETA inaendelea na mazungumzo na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa lengo la kutumia kanzidata yake katika kutambua watu walio katika mazingira magumu, hatua itakayosaidia kurahisisha upatikanaji wao kwa ajili ya mafunzo ya ufundi stadi.
Amesema ushirikiano huo pia unalenga kutafuta rasilimali kwa pamoja ili kuwezesha mafunzo na uendelezaji wa ujuzi kwa watu walio katika mazingira magumu, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha makundi yote yanapata fursa ya kushiriki katika shughuli za maendeleo.
“Juhudi zote hizo zinatoa mchango muhimu katika utekelezaji wa dhana ya ujumuishi katika ujuzi na uchangiaji wa makundi yote katika maendeleo ya nchi kiuchumi,” amesema Kasore.

Aidha, amesema VETA inatarajia kutoa mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana 14,000 kupitia mradi wa ushirikiano na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), hatua inayolenga kuongeza fursa za vijana kupata ujuzi na kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
Amesema kupitia hatua hizo, VETA inalenga kuendelea kuwa chombo muhimu katika kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi itakayochangia ujenzi wa uchumi imara, jumuishi na shindani unaolengwa na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

More Stories
Wafanyabiashara watakiwa kupanua biashara zao
Bandari ya Dar yazidi kung’ara
Kunenge:siamini katika kushindwa