Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imesema Bandari ya Dar es Salaam imeendelea kuongeza uwezo wa kupokea na kuhudumia mizigo kutokana na maboresho ya miundombinu na uwekezaji unaolenga kuongeza ufanisi wa shughuli za bandari.
Akizungumza wakati wa ziara ya viongozi wa wanafunzi wa vyuo vikuu katika miradi mbalimbali ya TPA, Mkurugenzi wa Huduma za Uhandisi wa TPA, Mhandisi Erick Madinda, amesema ongezeko la mizigo limeifanya mamlaka hiyo kuendelea kuboresha magati pamoja na miundombinu mingine ya bandari.
“Kwa sasa Bandari ya Dar es Salaam inahudumia kiasi kikubwa cha mizigo ambacho kimefikia takribani tani milioni 33.7. Hii inaonesha namna ambavyo mahitaji ya huduma za bandari yanavyoendelea kuongezeka,” amesema Madinda.
Amesema TPA inaendelea kuweka mikakati ya kuongeza uwezo wa bandari na kuhakikisha meli zinahudumiwa kwa muda mfupi ili kuongeza ufanisi wa biashara na kupunguza gharama zinazotokana na meli kukaa muda mrefu bandarini.

“Miongoni mwa miradi tunayotekeleza ni ujenzi wa matanki 15 ya kupokea na kusambaza mafuta. Mradi huu unatarajiwa kupunguza muda wa meli za mafuta kukaa bandarini kutoka hadi siku 21 hadi takribani siku saba,” amesema.
Kwa mujibu wa Madinda, hatua hiyo itasaidia kupunguza gharama za demurrage, ambazo zinaweza kufikia takribani dola 25,000 kwa siku kwa meli moja.
“Gharama hizi zinapungua kadri tunavyopunguza muda wa meli kukaa bandarini. Hii itasaidia kupunguza gharama kwa waagizaji wa mafuta na hatimaye kuchangia upatikanaji wa mafuta kwa gharama nafuu zaidi,” amesema.

Aidha, amesema TPA inaendelea na mipango ya kuongeza uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kwa kujenga na kuboresha magati, kuongeza uwezo wa kupokea meli kubwa pamoja na kuimarisha usafirishaji wa mizigo kupitia reli ya SGR na barabara.
“Lengo letu ni kuhakikisha Bandari ya Dar es Salaam inakuwa na ufanisi zaidi, inaongeza mapato na inatoa huduma bora kwa Tanzania pamoja na nchi nyingine zinazotegemea bandari hii,” amesema Madinda.

Kwa upande wao, viongozi wa wanafunzi waliotembelea bandari hiyo, Oswad Maganya, Rais wa Chuo Kikuu cha Ardhi, na Caren Mary, Makamu wa Rais wa Serikali ya Wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wamesema ziara hiyo imewapa fursa ya kujifunza kuhusu historia ya maendeleo ya Bandari ya Dar es Salaam pamoja na mipango yake ya baadaye.
“Ziara hii imetupa fursa ya kuona kwa vitendo namna Bandari ya Dar es Salaam inavyofanya kazi na kuelewa mchango wake katika uchumi wa taifa,” amesema Maganya.
Caren amesema maarifa waliyoyapata yatawasaidia kuongeza uelewa kuhusu nafasi ya bandari katika kurahisisha biashara na usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya Tanzania.
“Tumepata maarifa ambayo tunaamini yatatusaidia katika masomo yetu na pia kutufanya kuelewa zaidi mchango wa bandari katika maendeleo ya nchi,” amesema.
Wameongeza kuwa Bandari ya Dar es Salaam ina mchango mkubwa katika kurahisisha biashara na usafirishaji wa mizigo, hivyo uwekezaji unaoendelea katika miundombinu yake ni muhimu kwa uchumi wa Tanzania na nchi jirani zinazotumia bandari hiyo.

More Stories
WMA yatahadhari wanaochezea mizani
Wafanyabiashara watakiwa kupanua biashara zao
VETA yaweka mkakati kufikia Dira ya Taifa 2050