September 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wafanyabiashara watakiwa kupanua biashara zao

Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online, Mwanza

NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo amewataka wafanyabiashara hapa nchini kutumia fursa zilizopo kupanua shughuli zao, kuongeza uzalishaji na kutafuta masoko mapya ndani na nje ya nchi.

Huku taasisi za Serikali zinazohusika na usajili,viwango, kodi, biashara, uwekezaji na huduma nyingine zina wajibu wa kuwahudumia na kuwawezesha wafanyabiashara kukua kwa kutoa elimu, ushauri na huduma kwa wakati,ili wafanyabiashara hao waweze kufuata taratibu na kukuza biashara zao, badala ya kuonekana kama taasisi zinazolenga kuwakamata na kuwaadhibu.

Hayo yamezungumza Septemba 3,2026 , wakati akifungua Maonesho ya 21 ya Biashara ya Afrika Mashariki ya mwaka 2026 yaliyoandaliwa na Chemba ya Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo Tanzania(TCCIA) Mkoa wa Mwanza yanayoendelea katika Viwanja vya Furahisha wilayani Ilemela mkoani hapa.

Ambapo amesema,mfanyabiashara mwenye kiwanda kidogo leo anaweza kuwa na ndoto ya kukikuza na kukifanya kiwanda kikubwa kinachoweza kumilikiwa na vizazi vijavyo, huku uzalishaji wake ukifikia masoko ya Tanzania, Afrika na dunia kwa ujumla.

Aidha,amewataka wazalishaji kutambua kuwa ubora wa bidhaa si gharama, bali ni tiketi muhimu ya kuingia katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Amesema wazalishaji wanaoshiriki katika maonesho hayo wanapaswa kutumia huduma zinazotolewa na taasisi mbalimbali za Serikali zinazohusika na viwango,vipimo,usalama wa bidhaa na usajili wa biashara ili kuhakikisha bidhaa zao zinakuwa tayari kushindana katika masoko ya Afrika na dunia.

Hata hivyo amesema,wafanyabiashara wanahitaji mazingira rafiki ya kuanzisha na kuendesha biashara, ndiyo maana Wizara ya Viwanda na Biashara inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha sekta hiyo.

Baadhi ya hatua hizo ni pamoja na kutengeneza sera mpya inayogusa biashara na wajasiriamali wadogo, kurahisisha taratibu za kuanzisha na kuendesha biashara,kupunguza urasimu na gharama zisizo za lazima,kuimarisha mifumo ya kidijitali katika huduma za Serikali na kuwezesha upatikanaji wa taarifa za masoko.

“Tunataka mfanyabiashara atumie muda mwingi zaidi kufanya biashara na si kutumia muda mwingi kushughulikia urasimu wa taratibu zisizo za lazima katika ofisi za Serikali,”amesema Londo.

Kwa upande wake,Rais wa Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC), Vincent Minja,amesisitiza umuhimu wa wafanyabiashara kutumia maonesho hayo kujenga uhusiano mpya wa kibiashara na kutafuta masoko yatakayosaidia kukuza biashara zao.

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa (MNEC)Dkt. Angeline Mabula amesema,wafanyabiashara wanapaswa kuwa sehemu ya juhudi za kukuza uchumi kwa kutumia fursa zinazotokana na ongezeko la biashara ndani na nje ya nchi,huku akisitiza umuhimu wa sekta binafsi kushirikiana na Serikali katika kuibua fursa mpya za ajira na kuongeza uzalishaji na wafanyabiashara wadogo na wa kati kujenga uwezo wa biashara zao kwa kutumia teknolojia na ubunifu.

Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Amir Mkalipa, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza amesema Serikali imeendelea kutambua umuhimu wa kulinda biashara na kuhakikisha wafanyabiashara wanapata mazingira yanayowawezesha kufanya kazi na kunufaika na uwekezaji wao.

Mwisho.