
Na Moses Ng’wat, Songwe
MKUU mpya wa Mkoa wa Songwe, Abubakari Kunenge, amemshukuru, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumhamishia katika Mkoa huo, akiahidi kufanya kazi kwa bidii, haki na kuleta matokeo, huku akisisitiza kuwa yeye haamini katika kushindwa.
Kunenge ametoa kauli hiyo, Septemba 4, 2026, baada ya kukabidhiwa rasmi ofisi na kuanza majukumu yake, akisema kuhamishiwa kwake mkoani humo kunampatia jukumu kubwa la kuhakikisha wananchi wanahudumiwa.
Amesema anataka kuona wataalamu na watendaji wakitekeleza majukumu yao kwa weledi na kuzingatia misingi ya taaluma na kila mmoja anapaswa kuwajibika katika eneo alilokabidhiwa.

Aidha, amesisitiza matumizi ya takwimu katika kupima utekelezaji wa majukumu waliyokabudhiwa.
Kunenge pia amehimiza ushirikiano miongoni mwa viongozi, watendaji na wananchi, akisema mafanikio ya Mkoa wa Songwe yatategemea uwajibikaji wa kila mmoja na kufanya kazi kwa lengo moja.
“Nimekuja hapa kufanya kazi…. mimi si mtu wa kona kona, lakini nitamwomba Mungu anisaidie kufanya kazi kwa kutenda haki” amesema Kunenge.
Kwa upande wake, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Jabiri Omari Makame, alisema katika siku 427 alizohudumu mkoani humo, amebaini kuwa wananchi wake ni wakarimu na wachapakazi, akieleza kuwa Songwe ni mkoa wenye fursa na baraka kubwa.

Makame alisema Songwe imeendelea kuwa miongoni mwa mikoa kinara katika uzalishaji wa chakula, akieleza kuwa katika msimu wa kilimo wa 2025/26, mkoa huo ulizalisha tani milioni 1.7 za chakula, huku mahitaji yakiwa tani milioni 3.9.
Mwenyekiti wa Wakuu wa Wilaya Mkoa wa Songwe na Mkuu wa Wilaya ya Ileje,
Farida Mgomi, amempongeza Makame kwa uongozi wake uliolenga kuwaunganisha viongozi, watendaji na wananchi, akisema ameacha alama ya mshikamano katika kipindi cha uongozi wake.
Mgomi pia alimkaribisha Kunenge na kumwahidi ushirikiano wa Wakuu wa Wilaya katika kutekeleza majukumu yake, akisisitiza kuwa viongozi hao wako tayari kushirikiana naye kuhakikisha miradi na shughuli za maendeleo zinatekelezwa kwa manufaa ya wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Songwe amesema mabadiliko ya viongozi ni sehemu ya utaratibu wa kawaida.
Hata hivyo, amemtakaMkuu wa Mkoa mpya, Kunenge kuhakikisha anasimamia upatikanaji wa mbolea kwa wakati na kudhibiti utoroshwaji wake kwenda nchi jirani.

More Stories
Msai awataka wazazi kuchangia chakula kuwaepusha na ukatili
ALAF yaweka rekodi mpya kwenye tuzo za PMAYA
Makamba:Mradi Mpomvu,GGM kuimarisha upatikanaji umeme Geita