September 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Msai awataka wazazi kuchangia chakula kuwaepusha na ukatili

Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOnline, Mbeya

WAZAZI na walezi Jijini Mbeya wametakiwa kuhakikisha wanachangia chakula shuleni, ili wanafunzi wapate mahitaji muhimu wanapokuwa masomoni na kuepuka mazingira hatarishi yanayoweza kuwaweka katika hatari ya kukumbana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Rai hiyo imetolewa Septemba 3, 2026 na Diwani wa Viti Maalum Jiji la Mbeya, Atupele Msai, wakati akikabidhi msaada wa chakula katika Shule ya Msingi Isanga, akisema hatua hiyo inalenga pia kuhamasisha wazazi na walezi kutambua wajibu wao katika kuhakikisha watoto wanapata chakula shuleni.

Msai amesema chakula ni sehemu muhimu ya ustawi wa mwanafunzi kwa kuwa humwezesha kuwa na utulivu na nguvu za kushiriki kikamilifu katika masomo, huku akisisitiza kuwa wazazi wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha mahitaji hayo yanapatikana.

“Chakula nilichotoa ni kwa ajili ya kusaidia watoto wetu. Ndugu wazazi na walezi, tujitahidi kuwa mfano katika kuchangia chakula ili watoto wetu wapate mahitaji hayo muhimu, waepuke mazingira hatarishi na waweze kumudu vipindi vyao vya masomo,” amesema Msai.

Amesema ushirikiano kati ya wazazi, walezi na shule ni muhimu katika kulinda ustawi wa watoto, akieleza kuwa jukumu la kuhakikisha mwanafunzi anapata mahitaji ya msingi haliwezi kubebwa na shule pekee.

Katika hatua hiyo, madiwani Magreth Kalonga na Fatuma Bora wameungana na Msai katika zoezi hilo, huku wakitoa wito kwa jamii kuendelea kushirikiana katika kuhakikisha watoto wanapata chakula shuleni.

Wamesema mchango wa jamii katika upatikanaji wa chakula unaweza kusaidia kuboresha ustawi wa wanafunzi, usalama wao na mazingira ya kujifunzia, hasa kwa watoto wanaotoka katika familia zenye changamoto.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Isanga, Kissa Kibona, amemshukuru Msai kwa msaada huo na kuwasihi wazazi na walezi kutimiza wajibu wao wa kuchangia chakula kwa ajili ya wanafunz

Kibona pia amewataka wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi, ili kuwawezesha kupata mahitaji muhimu na kuendelea na masomo katika mazingira salama na yenye staha.