September 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ALAF yaweka rekodi mpya kwenye tuzo za PMAYA

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

KAMPUNI ya kutengeneza mabati ya ALAF imeendelea kuonyesha ubora na ushindani katika sekta ya viwanda nchini baada ya kuibuka mshindi wa kwanza katika kipengele cha Chuma na Bidhaa za Chuma kwenye Tuzo za Rais za Mzalishaji Bora wa Mwaka (PMAYA), toleo la 19.

Ushindi huo unaifanya ALAF kuendeleza rekodi yake ya kutwaa tuzo hiyo kwa mara ya 17 mfululizo tangu ilipoanza kushiriki katika tuzo hizo zinazolenga kutambua na kuenzi wazalishaji wanaofanya vizuri katika sekta mbalimbali za viwanda.

Tuzo hiyo ilikabidhiwa na Makamu wa Rais, Deogratias Ndejembi, katika hafla iliyowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya viwanda nchini.

Tuzo za PMAYA hutolewa na kuratibiwa na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kutambua mchango wa wazalishaji katika kukuza sekta ya viwanda, kuongeza ushindani na kuchochea maendeleo ya uchumi wa Tanzania.

Akizungumza baada ya ushindi huo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa ALAF, Hawa Bayumi, amesema tuzo hiyo ni kielelezo cha dhamira ya kampuni hiyo katika kuhakikisha inazalisha bidhaa zenye viwango vya ubora vinavyokubalika kimataifa.

“Tuzo hii inadhihirisha uwajibikaji wetu katika kuzalisha kwa viwango bora duniani, kuwa mstari wa mbele katika uvumbuzi na kuwa sehemu ya ukuzaji wa viwanda Tanzania,” amesema Bayumi.

Amesema ushindi huo pia unaonyesha matokeo ya juhudi za pamoja za wafanyakazi wa ALAF, washirika pamoja na wateja wanaoendelea kuiamini kampuni hiyo katika shughuli zao za ujenzi.

Bayumi ametoa shukrani kwa CTI kwa kuendelea kuandaa tuzo hizo, huku akiishukuru timu nzima ya ALAF kwa kujituma na kuhakikisha kampuni inaendelea kushindana na kufanya vizuri katika sekta ya viwanda.

Aidha, amewashukuru wateja wa ALAF kwa kuendelea kuiamini na kuunga mkono kampuni hiyo katika safari yake ya uzalishaji na utoaji wa bidhaa za chuma.

“Asanteni kwa kutuunga mkono na imani yenu kwetu. Pamoja tutaendelea kujenga viwanda imara, jamii imara na Tanzania imara zaidi,” amesema.

Ushindi huo unaendelea kuiweka ALAF katika nafasi ya muhimu katika sekta ya uzalishaji wa bidhaa za chuma nchini, huku rekodi ya kutwaa tuzo mara 17 mfululizo ikionyesha mwendelezo wa kampuni hiyo katika ubora, ubunifu na uzalishaji.

Kwa ALAF, tuzo hiyo ni zaidi ya ushindi wa kampuni, bali ni sehemu ya mchango wake katika kuimarisha sekta ya viwanda na kusaidia kujenga Tanzania yenye uzalishaji na ushindani mkubwa.