August 31, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tabora kulipa mil.27 za HESBL

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online,Tabora

HALMASHAURI ya Manispaa Tabora imetenga jumla ya sh.milioni 27 kwa ajili ya kuwalipia watumishi wake waliosoma vyuo vikuu kwa fedha za mkopo wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kabla ya kuajiriwa.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora Dkt.John Pima wakati akitoa taarifa ya hesabu za mwisho (final accounts) kwenye kikao cha Baraza la Madiwani adiwani wa halmashauri hiyo.

Amesema,halmashauri hiyo imetenga kiasi hicho katika bajeti yake ya mwaka huu ili kuwezesha watumishi wake walionufaika na mkopo wa Serikali unaotolewa na HESLB kurejesha mikopo yao kwa wakati.

“Haya ni maelekezo ya Serikali kwa waajiri wote nchini,kuhakikisha wanatambua watumishi wao waliosoma kwa fedha za mkopo wa bodi hiyo na kurejesha sehemu ya mikopo yao kila mwaka,”ameeleza.

Dkt.Pima amesema,wamekuwa wakifanya hivyo kila mwaka ili kuhakikisha kila mtumishi anamaliza marejesho ya mkopo wake ili kuiwezesha bodi hiyo kuendelea kukopesha wanafunzi wengine wenye uhitaji wa mkopo huo wa elimu.

Pia amesema wametenga zaidi ya sh.milioni 379 kwa ajili ya kulipa madeni ya stahiki mbalimbali za watumishi wa halmashauri hiyo wasio walimu ili kuwaongezea ari ya kufanya kazi kwa weledi.

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora Ghullam-Hussein Remtullah amesisitiza kuwa mafanikio ya halmashauri hiyo yanachochewa na mshikamano mzuri uliopo kati ya Mkurugenzi,watalaamu, watendaji na Madiwani, hivyo ameomba mshikamano huo uendelee ili kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella amepongeza halmashauri hiyo kwa kuendelea kuandaa vizuri taarifa za hesabu zake za mwaka hali ambayo imesaidia kupata hati safi mfululizo.

Akitoa angalizo la mvua za El-nino, Wella ameagiza halmashauri na taasisi husika zote kuhakikisha miundombinu ya barabara zote inasafishwa mapema ikiwemo kuzibua mifereji na mitaro ya kupitisha maji ili kuepusha mafuriko mvua zitakapoanza kunyesha.